RAIS Jakaya Kikwete ameagiza ripoti maalumu ya tathimini ya rushwa nchini, iliyofanywa na Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), itolewe hadharani ili wananchi waijadili.
Ametoa agizo hilo mjini Dodoma katika kikao cha kusaini mkataba wa makubaliano kati ya Serikali na washirika wa maendeleo wanaotoa misaada moja kwa moja katika bajeti (GBS), Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema ripoti hiyo itatolewa wakati wowote kuanzia sasa.
Kwa mujibu wa Pinda, washirika hao wa maendeleo walitoa fedha kwa ajili ya kutathimini hali ya rushwa nchini kuanzia katika ngazi ya familia, kazi iliyomalizika mwaka 2009.
"Walifanya tathmini kuanzia huko vijijini, katika upatikanaji wa huduma za umma za afya, elimu maji na nyingine...sina hakika walikwenda mpaka katika ngazi gani ya juu lakini imeonesha tatizo bado ni kubwa," amesema Pinda.
Baada ya kukamilika kwa tathimini hiyo, Pinda alisema, ripoti hiyo, ambayo taarifa nyingine zilieleza iliandaliwa na Takukuru, ilipelekwa serikalini lakini ilikuwa haijajadiliwa katika Baraza la Mawaziri.
"Lakini Rais Kikwete kasema si lazima ingoje Baraza la Mawaziri, kaagiza niichapishe wananchi waione kwa kuwa inagusa maeneo mengi ya jamii," alisema na kuongeza kuwa itasaidia serikali kukaza uzi katika maeneo ambayo inalegalega.
Baada ya kauli hiyo, Mwenyekiti wa washirika wa maendeleo, zikiwemo baadhi nya nchi na mashirika ya fedha yanayotoa msaada wao moja kwa moja katika bajeti, Balozi Ingunn Klepsvik wa Norway, alisifu hatua hiyo ya Rais Kikwete na kuongeza kuwa itasaidia kuongeza mapambano dhidi ya ruswa.
Hata hivyo balozi huyo alisisitiza kuwa, mapambano dhidi ya rushwa, yalionesha mwelekeo mzuri mpaka mwaka 2007, lakini baada ya hapo hakuna ushahidi unaoonesha serikali imepiga hatua katika mapambano hayo.
"Kulitokea kesi kubwa za rushwa kati ya 2007 na 2008 na serikali ikachukua hatua zilizosababisha wahisani kuwa na imani, lakini hakuonekani kasi katika kumaliza baadhi ya hizo kesi hizo.
"Kama kesi hizo zikiharakishwa na haki ikaonekana, tutapiga hatua kubwa ya kupambana na rushwa na kujenga imani kubwa ya kuendelea kutoa misaada kupitia mfumo huu wa kuchangia bajeti moja kwa moja," alisema Balozi Klepsvik.
Balozi Klepsvik alikumbusha kuwa mwaka jana, wadau wa maendeleo waliona kuwa hakukuwa na hatua za kuridhisha katika makubaliano ya kupambana na rushwa kati yao na serikali.
Kutokana na hali hiyo isiyoridhisha, Balozi Klepsvik alisema washirika hao wa maendeleo waliomba kuwepo majadiliano kati yao na serikali ambayo yameanza.
Majadiliano hayo kwa mujibu wa Balozi Klepsvik, pia yatatathimini maendeleo ya vita dhidi ya rushwa kwa kuwa bila ushahidi usio na mashaka kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanapamba moto, itakuwa vigumu kushawishi nchi zao nkuwa mfumo wa kutoa misaada moja kwa moja katika bajeti ni mzuri.
Kutokana na umuhimu huo, makubaliano ya kuendelea kutoa msaada kupitia mfumo huo kwa miaka mitano ijayo yaliyosainiwa jana kati ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo na washirika hao 12 wa maendeleo, pia yamesisitiza umuhimu wa kuendelea na mapambano dhidi ya rushwa.
0 Comments