WATU 10,000 watanyang’anywa viwanja wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam baada ya kubainika kuvamia maeneo ya watu kinyume cha sheria na kuyafanya makazi yao ya kudumu.

Akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Modeye, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana, alisema, wilaya hiyo ina tatizo la uvamizi linalosababisha kuibuka kwa migogoro mingi ya ardhi.

Rugimbana alisema hekta zaidi ya 1,000 zilizoko katika wilaya yake zimevamiwa na watu hao na sasa Serikali wilayani humo imeamua kulivalia njuga suala hilo kuhakikisha Sheria ya Ardhi inafuatwa. 

Alisema, wilaya hiyo imeamua kushirikisha uongozi wa Mkoa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi katika utatuzi wa migogoro hiyo kwa kushirikisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo kutokana na migogoro mingi kusababisha kuwepo kwa mapigano.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema mapendekezo watakayoyatoa watayawasilisha mkoani na wizarani ili washirikiane kuyatafutia ufumbuzi matatizo hayo ya uvamizi.


Rugimbana aliwalaumu viongozi wa Serikali za Mitaa kuwa ndiyo wahusika wakuu wa kuuza maeneo yanayomilikiwa na watu kisheria na kusababisha watu kuyavamia na kuyafanya maeneo yao ya kuishi.


Aliyataja baadhi ya maeneo ambayo yamevamiwa kuwa ni Madale, Kilimahewa, Mivumoni, Chasimba katika eneo la kiwanda cha saruji cha Twiga na Mbezi Juu ambako alisema katika maeneo hayo, kuna migogoro inayohatarisha usalama na maisha ya watu.


“Tayari Wilaya tumependekeza namna ya kutatua migogoro hii na kesho (leo) Kamati ya Ulinzi na Usalama itakaa kuona namna ambavyo uongozi wa Mkoa na Wizara watashiriki kutafuta ufumbuzi,” alisema Rugimbana.


Licha ya tatizo hilo la kuvamiwa kwa maeneo ya watu, lakini Rugimbana pia alisema wilaya yake inakabiliwa na mgogoro kati ya mtu na mtu mahali ambako kiwanja kimoja kimemilikishwa kwa watu zaidi ya mmoja.


Ole Modeye Jumanne na Jumatano atatembelea baadhi ya maeneo yanayodaiwa kuvamiwa na watu na kujenga nyumba za kuishi na hawataki kutoka.


Akizungumza na wanahabari kabla ya kuanza ziara yake, Ole Modeye alisema Serikali haiwezi kutatua migogoro hiyo kwa kutumia nguvu, bali watakaa na pande zinazohusika ili suluhisho lipatikane.


Alisema wizara yake kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa pamoja na Wilaya ya Kinondoni, wamejipanga kuhakikisha migogoro hiyo ya ardhi inamalizika na mwenye haki ya kumiliki eneo husika anapewa eneo lake.


“Kama kuna mtu alimilikishwa eneo kisheria ndiye mwenye haki na Serikali itamlinda,” alisema Naibu Waziri huyo ambaye alisisitiza kuwa kabla ya uamuzi kuchukuliwa kila upande utashirikishwa kwa majadiliano.


Alisema, sheria inakataza kuwaadhibu watu bila kuwahoji au kuwapa fursa ya kusikilizwa na yeye anafanya ziara hiyo kuhakikisha maeneo yote yenye migogoro yanapatiwa ufumbuzi.


Pia Naibu Waziri huyo aliungana na hoja ya DC wa Kinondoni kuwa baadhi ya watendaji wa Serikali za Mitaa wamekuwa wakishirikiana na wavamizi kuchukua maeneo hayo na kuchangia kuwepo kwa migogoro mingi ya ardhi katika eneo hilo.


Migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Kinondoni imesababisha hivi karibuni watu wawili kuuawa na wengine kujeruhiwa vibaya baada ya mtu anayedaiwa kuwa mmiliki halali wa eneo la Mivumoni kupeleka vijana kwa ajili ya kuvunja nyumba za wavamizi wa eneo analodai kulimiliki.


Hata hivyo watuhumiwa wa uvamizi huo ambao ni wananchi waliojenga maeneo yao ya kudumu katika eneo hilo, waliwazidi nguvu vijana hao na kuwaua wawili na kuwajeruhi wengine kadhaa.