Aliyekuwa rais Nelson Mandela amepiga kura nyumbani nchini Afrika kusini katika uchaguzi mdogo, siku mbili kabla, kama wengine ambao hawawezi kufika kwenye vituo vya kupiga kura.
Wakfu wake ulitoa picha zake kwa mara ya kwanza za shujaa huyo mwenye umri wa miaka 92 aliyepambana na ubaguzi wa rangi tangu alipokuwa amelazwa hospitalini mwezi Januari.
Alifuatana na mkewe, mtoto wake wa kike na mjukuu wake.
Hakuwahi kutokea hadharani tangu sherehe za kumalizika kwa Kombe la dunia Julai 2010.
Waandishi walisema anazidi kuonekana dhaifu mara chache anazoonekana tangu kujiuzulu kuonekana hadharani mwaka 2004.

Bw Mandela, anayejulikana na raia wa Afrika kusini kwa jina lake la ukoo Madiba, alifungwa gerezani miaka 27 na serikali iliyokuwa ikifuata sera za ubaguzi wa rangi.
Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel aliachiwa huru mwaka 1990 na kukiongoza chama cha African National Congress ANC katika ushindi wa kishindo mwaka 1994- mara ya kwanza kwa watu weusi walio wengi kuruhusiwa kupiga kura.
Aling'atuka kama rais mwaka 1999 lakini ANC imeweza kuendelea kuwa na wanachama wengi kwenye bunge la nchi hiyo.