MFUKO wa Pensheni wa PPF umetumia Sh milioni 371.2 kwa mwaka huu pekee, kuwasomesha watoto yatima 1,075 ambao wazazi wao wamefariki dunia wakiwa wanachama wa mfuko huo.
Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mkuu wa PPF, William Erio wakati wa semina ya uongozi wa Mfuko huo na wahariri wa vyombo vya habari nchini iliyofanyika jijini hapa.
Erio alisema watoto hao wanalipiwa ada za shule ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mafao ya elimu, moja ya mafao saba yanayotolewa na mfuko huo.
Watoto wa wazazi ambao walikuwa wanachama wa mfuko huo, lakini wakafariki dunia, hulipiwa ada ya kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne.
Mbali ya mafao ya elimu, mafao mengine ya PPF ni Mafao ya Uzeeni, Malipo ya Kiinua Mgongo, Malipo ya Kifo, Malipo ya Wategemezi, Mafao ya Ugonjwa na Mafao ya Kujitoa.
Akifafanua, Erio alisema PPF hutoa malipo hayo kwa watoto wanne wa familia ya mwanachama aliyefariki dunia na kwamba kuanzia sasa, itakuwa inafuatilia maendeleo yao shuleni na hata katika mitihani ya kitaifa ili Mfuko utambue mafanikio yao.
“Katika hili, lazima tujivunie kwamba tunaijali jamii, ndiyo maana tumekuwa tukitumia fedha nyingi kuwasomesha watoto wa wanachama wetu waliofariki dunia.Kwa mfano mwaka huu pekee tumetumia shilingi 371,255,002.56. “Hii ni sehemu ya faida inayorudi kwa wanachama wetu.
Kuwa yatima haina maana hauna thamani, kwetu PPF, hawa wana umuhimu ndiyo maana tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanapata elimu,” alisema Erio.
Alisema kutokana na michango na faida kutokana na uwekezaji katika sekta mbalimbali, PPF kwa sasa ina uwezo wa kujiendesha bila kutetereka hadi mwaka 2056, yaani kwa miaka 45 kuanza sasa.
Mbali ya majengo ya vitegauchumi katika majiji ya Dar es Salaam, Mwanza na Arusha, PPF inakusudia kusambaza miradi zaidi katika sehemu mbalimbali nchini, na kujenga nyumba za bei nafuu na kuziuza ili pamoja na kuboresha uwezo wa kifedha wa Mfuko, isogeze pia huduma za kijamii karibu na wananchi.
0 Comments