KIUNGO Nizar Khalfan hatakuwemo kwenye kikosi cha timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kitakachocheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ Jumamosi. 
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa, hatua hiyo inatokana na timu yake ya Vancouver Whitecaps kumnyima ruhusa kwa vile Mei 15 mwaka huu itakuwa na mechi muhimu ya ligi.

“Ujio wa wachezaji Idrissa Rajab, Henry Joseph, Abdi Kassim, Dan Mrwanda na Athuman Machupa bado tunafuatilia majibu katika klabu zao,” alisema Wambura akizungumzia wachezaji wengine wanaocheza soka nje ya Tanzania.


Alisema, maandalizi kuhusiana na mchezo huo yanakwenda vizuri na kuwa kikosi cha Bafana Bafana kikiongozwa na kiungo wa Kaizer Chiefs, Siphiwe Tshabalala kitawasili nchini kesho saa 1:30 usiku kwa ajili ya mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Aliwataja wachezaji wengine kwenye kikosi hicho kinachofundishwa na Pitso Mosimane kuwa ni makipa: Itumeleng Khune na Wayne Sandilands. Mabeki ni Morgan Gould, Siyanda Xulu, Eric Matoho, Mzivukile Tom, Prince Hlela, Siyabonga Sangweni, Tefu Mashamaite na Siyanda Zwane.


Viungo ni Hlompho Kekana, Thanduyise Khuboni, Reneilwe Letsholonyane, Thandani Ntshumayelo,Thabo Matlaba, Erwin Isaacs na Sifiso Myeni wakati washambuliaji ni Bernard Parker, Vuyisile Wana, Lehlohonolo Majoro na Katlego Mphela.


“Tiketi kwa ajili ya mchezo huo zitaanza kuuzwa Alhamisi katika vituo vya Premier Betting (Kariakoo- Mtaa wa Sukuma, Buguruni Sokoni, Manzese Midizini, JM Mall na Tandale kwa Mtogole), Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Steers (Mtaa wa Ohio na Samora), Big Bon Msimbazi (Kariakoo) na Uwanja wa Uhuru,” alisema Wambura.