Shinikizo la kuwataka viongozi wa ngazi ya juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwajibika wenyewe kwa kujiondoa katika nafasi zao kutokana na tuhuma za ufisadi kama Halmashauri ya Taifa (NEC) ya chama hicho ilivyoazimia, linazidi kuongezeka.
Moja ya mazimio ya NEC katika kikao chake kilichomalizika Aprili 11, mwaka huu mjini Dodoma liliwataka watuhumiwa wenye kashfa za ufisadi kutafakari, kupima na kuamua kujiwajibisha kabla chama hicho hakijawawajibisha kwa lengo la kukirejesha katika maadili.
Mjumbe wa NEC, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema wanachama wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi wakubali maamuzi yaliyofikiwa na chama kwa kuchukua hatua kujiwajibisha kwani tuhuma zinazowakabili hazihitaji kuthibitishwa na mahakama kwa sababu dhamana ya uongozi kisiasa haifanani na ajira ya serikali.
Dk. Mwakyembe ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Kyela, mkoani Mbeya, alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa kata za Ngonga na Ikolo zilizopo jimboni mwake katika mikutano ya hadhara aliofanya siku ya kwanza ya ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo ambako alitumia fursa hiyo kuelezea maana ya CCM kujivua gamba. Alisema kumezuka maneno kutoka kwa baadhi ya watu ambao wanadai kwamba wanachama wa CCM wanaotakiwa kujiondoa katika nafasi za uongozi wa chama katika kutekeleza dhana ya kujivua gamba wanaonewa kwa sababu tuhuma dhidi yao hazijathibitishwa.
Alisema wanaotoa madai hayo kwa sababu hawaelewi kwamba dhamana ya uongozi kisiasa ni tofauti na ajira ya serikali.
Dk. Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema kwenye dhamana ya uongozi wa kisiasa haihitaji tuhuma yoyote ile ambayo wananchi wanahisia nayo ithibitishwe kimahakama badala yake hisia tu inatosha kwa mtuhumiwa kuwajibika au kujivua gamba na bila kufanya hivyo mhusika anakuwa anakiumiza chama chake.
" Dhamana ya uongozi kisiasa haifanani na ajira ila kama umeajiriwa serikalini una tuhuma ya wizi, lazima anayekutuhumu kwa wizi athibitishe, na unatafuta na mashahidi, lakini kwenye siasa ushahidi hauthibishwi ilimradi wananchi wamekuhisi kaa pembeni uwanusuru wenzako," alisema.
Alisema kutokana na tuhuma hizo zinazotokana na hisia, hata kama mtuhumiwa ajisafishe kiasi gani ataendelea kuchafuka mbele ya wananchi na ndiyo maana wananchi hukumu yao huwa wanaitoa wakati wa uchaguzi ambayo inatokana na hisia na wala siyo mambo ambayo yamethibitishwa na mahakama.
" Tuhuma za hisia kisiasa hata kama ujisafishe kiasi gani unaendelea tu kuchafuka mbele ya wananchi, na wananchi ndio wenye maamuzi na ndiyo maana hukumu ya mwananchi inatolewa wakati wa uchaguzi na hukumu yao inatokana na hisia na wala siyo mambo ambayo yamethibitishwa na mahakama na ukisubiri hadi ithibitishwe na mahakama unajitafutia shida kwa wananchi," alisema Dk. Mwakyembe.
Aliongeza kuwa wanachama wa CCM lazima watambue kuwa kujivua gamba ni muongozo wa chama hicho wa mwaka 1981 kwa maana ya kujikosoa na kukosoana.
Alisema sehemu ya kura ambazo CCM ilizikosa kwa wananchi katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana ni kutokana na tuhuma za ufisadi dhidi ya baadhi ya wanachama ambazo ziliwafanya wananchi kufikiri kuwa wana-CCM wote ni mafisadi na wala rushwa wakati siyo kweli.
Alisema ndiyo maana msimamo wa chama ni kwamba wachache wanaotuhumiwa kwa ufisadi wakae pembeni.
Alisema suala la kujiuzulu au kujivua gamba ndani ya CCM halijaanza leo na kutolea mfano miaka ya sabini ambapo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Hassan Mwinyi, alijiuzulu kufuatia vifo vya watuhumiwagerezani mkoani Shinyanga kwa lengo la kukinusuru chama na serikali.
" Mwinyi alijiuzulu japo hakuwahi hata kuwaona hata wale watuhumiwa, wala kutoa amri ya kukamatwa kwao ila kwa kuwa watendaji wake wa chini ya wizara yake ndio walifanya huo ujinga akajiuzulu akikubali kuwa makosa yamefanyika chini ya wizara yake ambayo anaisimamia, kwa hiyo akakubali kujivua gamba na wananchi walifurahi sana," alisema Naibu waziri huyo.
Alitoa mfano mwingine kuwa mapema miaka themanini kulitokea kashfa nyingine ya mmoja wa watuhumiwa wa uhaini waliokuwa gereza la Ukonga ambaye alitoroka na kumlazimisha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Marehemu Said Abdallah Natepe, alijiuzulu na kuongeza kuwa huo ndio utamadauni wa kujivua gamba.
Dk. Mwakyembe, alisema kutokana na utamaduni huo ndiyo maana CCM inasema kuna watu ndani ya chama ambao umma unawanyoshea vidole kwa tuhuma za kashfa za Richmond, Dowans, Kagoda na Epa na kwamba wananchi wanawajua kwa hiyo hawanabudi kujivua gamba ili kukiokoa chama.

DK. KIGODA NAYE ANENA
Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) Dk. Abdallah Kigoda, amesema kuwa wamejivua gamba kuanzia ngazi ya juu na kwamba wimbi hilo litaendelea hadi chini ngazi ya nyumba kumi (ubalozi).
Kigoda, alisema lengo ni kuimarisha chama ili kiweze kurudisha imani kwa wananchi na kuwavutia wengi hasa vijana.
Aliyasema katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa soko la zamani katika mjini wa Chanika wilayani Handeni, wakati wa ziara yake ya kutembelea wilaya za Mkoa wa Tanga.
Dk. Kigoda ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Handeni na Mjumbe wa NEC, alisema kuwa: " Kuna msemo wa Kizigua unasema kondoo kurudi nyuma ni kukusanya nguvu. Natoa wito kwa wana-CCM nchini kote, itakua ni kosa kubwa na la aibu kama CCM itashindwa na kuitwa chama cha upinzani." “Wajua ushindani wa kisiasa ni mzuri, lakini wengine wanafanya kama ni ushindani wa kucheza kiduku kueneza propaganda za kuwagawa watanzania,” alisema.

CCM MPANDA WAUNGA MKONO MAAMUZI YA NEC
Katika hatua nyingine, wanachama wa CCM Wilaya ya Mpanda katika Mkoa wa Katavi wamefanya maandamano ya amani kuipongeza Sekterarieti ya chama hicho kwa uamuzi wake wa kuwataka wenye maadili mabaya ndani ya chama hicho kujiwajibisha.
Maandamano hayo yaliyofanyika mjini Mpanda na kushirikisha wanachama wa chama hicho yalikuwa na lengo la kuipongeza NEC kuridhia kujiuzulu kwa Seketarieti na kamati CC. Akizungumza baada ya maandamano hayo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa, Hypolitus Matete, alisema licha uvuaji wa magamba ndani ya chama hicho kuanza kwa viongozi wa ngazi za juu, wajumbe wa NEC Taifa waliazimia hilo lishuke hadi chini kwa wanachama wasiokuwa na maadili kwa lengo la kukijenga upya chama hicho.
Matete, alisema ni lazima ifike mahali wote wasio na maadili ndani ya chama kujiondoa wenyewe na tayari wamekwisha kupewa muda wa kufanya hivyo na wakigoma chama kitachukua hatua ya kuwafukuza.
Katibu wa CCM Wilaya ya Mpanda, Jacob Nkomola na mwakilishi wa wazee, John Kiliko, walisema kuwa lengo la maandamano hayo ya amani ni kuunga mkono jitihada za NEC pamoja na kumpongeza Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kwa kufafanua kuwa CCM si fisadi bali fisadi ni mtu yoyote asiye na maadili mema ndani ya jamii.
Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe, Kyela; Sonyo Mwenkale, Handeni na Mwandishi Wetu, Katavi.
CHANZO: NIPASHE