MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Ndege Nchini (ATCL) David Mattaka(Pichani juu) amestaafu rasmi utumishi wa umma.
Mattaka amemshukuru Rais mstaafu Benjamin Mkapa kwa kumfundisha maana ya maisha.
Mattaka aliyetimiza miaka 60 Mei 11 na kulazimika kuacha majukumu yake ATCL kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma, pia ameishauri Serikali iimarishe sekta ya anga kabla ya kualika wawekezaji, ili iwe msimamizi mkuu wa biashara ya usafiri huo nchini itakapotengemaa.
Akizungumza ofisini kwake Dar es Salaam jana, Mattaka alisema, “ninashukuru kwa kumaliza kipindi changu cha utumishi wa umma salama. Ninamshukuru pia Rais mstaafu Benjamin Mkapa kwa kunisafisha kutokana na tuhuma zilizokuwa zikinikabili na hivyo kusababisha nistaafu kwa heshima.
“Ingawa ninasikitika kuliacha shirika likiwa halijatengemaa kibiashara kutokana na hali mbaya ya kifedha inayolikabili, ninamshukuru Mkapa kwa kuniwezesha kutambua marafiki wa Mattaka kama Mkurugenzi Mkuu wa PPF na marafiki wa Mattaka kama Mtanzania wa kawaida … hili ni funzo kubwa nililolipata wakati aliponisimamisha kazi”.
Pamoja na kuwashukuru marais wastaafu marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa elimu ya bure iliyomwezesha kufikia alipo sasa, Ali Hassan Mwinyi kwa kumteua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa kwanza wa Mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya Umma (PPF) na Rais Jakaya Kikwete kwa kumpa ukurugenzi wa ATCL, Mattaka alisema hatamsahau Mkapa.
Alieleza kuwa mafanikio aliyoyasababisha PPF wakati shirika hilo likijitegemea akiwa Mkurugenzi Mkuu, ndiyo yaliyomletea misukosuko iliyomfanya Rais Mkapa wakati huo amsimamishe kazi kwa muda mrefu, ili kuruhusu uchunguzi wa tuhuma za rushwa na wizi zilizokuwa zikimkabili.
“Watu waliona magari yangu niliyokopa PPF na Benki ya Posta, wakaanza maneno na kashfa za rushwa na wizi wa mali ya umma, ndipo Mkapa akaamua kuruhusu uchunguzi na kuniweka pembeni.
“ Nilisimamia vitega uchumi vingi vilivyofanikiwa, lakini wenye kutengeneza tuhuma, kashfa na majungu, hawakujali hilo na ndipo Polisi, Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB) wakati huo, sasa Takukuru, wakaanza kunichunguza na kuleta majibu yaliyonisafisha”.
Alisema, kama Mkapa asingemwondoa kazini na kuagiza uchunguzi wa kina, hadi leo angekuwa akinyooshewa vidole, kusakamwa na kuitwa fisadi.
“Ninashukuru na nina furaha, nimestaafu kazi na si nguvu ya kufanya kazi, nimewajua marafiki wa kweli wakati wa shida na marafiki wa kufuata vyeo, yote haya ni mafunzo niliyoyapata kwa sababu ya Mkapa, nimewajua binadamu na nimejifunza kuishi na watu. Iliniuma kama binadamu kukaa benchi lakini baadaye nilijifunza mambo mengi zaidi”.
Katika hatua nyingine, alisema ATCL haina ndege zinazofanya kazi kwa sasa kwa sababu zipo katika matengenezo.
Aidha, aliizungumzia ndege iliyoko Afrika Kusini na kusema matengenezo yake yamekamilika na Serikali inasubiriwa itoe fedha ili ikagombolewe na kuanza safari zake mara moja.
Alipoingia ATCL mwaka 2007, Mattaka alisema alilikuta shirika hilo na madeni ya Sh bilioni 23, mtaji wa Sh bilioni 14, huku ruzuku ya Sh milioni 500 iliyokuwa ikitolewa na Serikali ikiwa imesitishwa na hakukuwa na fedha zozote zilizokuwa zikiingizwa ATCL.
William Haji ndiye atakayekaimu nafasi yake hadi atakapopatikana Mkurugenzi Mtendaji mwingine.
Wakati huo huo, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amemteua Patrick Mfugale, kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).
Kabla ya uteuzi huo, Mfugale alikuwa akikaimu nafasi hiyo na pia aliwahi kushika nafasi nyingine katika utumishi wa umma ikiwamo ya Mhandisi Mkuu mwenye majukumu maalumu katika Wizara ya Ujenzi. Pia aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Barabara za Mikoa na kusimamia ujenzi wa barabara na madaraja mengi nchini.
Mfugale ana Shahada ya Kwanza ya Uhandisi ya Chuo Kikuu cha Roorkee, India na Shahada ya Uzamili ya Chuo Kikuu cha Loughborough, Uingereza. Uteuzi huo ni wa miaka mitatu na ulianza Mei 20.
0 Comments