Rais wa Marekani Barack Obama amezuru eneo ambalo mashambulizi ya 11 Septemba yalitokea mjini New York.
Ziara hiyo inafanyika siku nne baada ya kuuawa kwa kiongozi wa kundi la Al-Qaeda Osama Bin Laden, nchini Pakistan.
Inaaminika Bin Laden ndiye aliyepanga mashambulizi hayo ya 9/11 mwaka wa 2001.
Rais Obama aliweka shada la maua kuwakumbuka takriban watu 3000 waliofariki na pia kuzungumza na jamaa zao katika eneo hilo.
Awali Obama aliwaambia maafisa wa kikosi cha kuzima moto kuwa: ''Wakati tunaposema hatuwezi tukasahau, tunamaanisha vivyo hivyo''.
Ziara hiyo inakuja siku moja baada ya rais wa Marekani kusema hatachapisha picha ya mwili wa Osama Bin Laden.
Kiongozi huyo wa Al-Qaeda aliuwawa na vikosi maalum vya jeshi la Marekani kaskazini mwa Pakistan siku ya Jumatatu.
Baadaye mwili wake ulizikwa kwenye bahari kutoka kwa ndege ya Marekani iliyokuwa imembeba.
Majeshi ya Pakistan yalikiri kushindwa kugundua alikojificha Bin Laden na kusema wataanzisha uchunguzi.
Pakistan pia imedokeza kuwa itatizama upya ushirikiano kati yake na Marekani iwapo kutatokea uvamizi mwingine bila ya wao kufahamishwa kama ilivyofanyika na Osama bin Laden.