TAASISI isiyo ya Kiserikali ya Twaweza imebaini mazingira ya kujifunzia yasiyoridhisha katika shule za msingi jijini Dar es Salaam, hali iliyoelezwa kuwa inadhihirisha sekta ya elimu ni tete nchini.

Twaweza ilitoa jana muhtasari wa utafiti ilioufanya katika shule 40 za msingi katika wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni kati ya Agosti na Desemba mwaka jana na kubaini kuwa zinakabiliwa msongamano madarasani, ukosefu wa madawati na ukosefu wa vitabu vya kiada.


“Watafiti wameonesha mashaka yao kuwa iwapo mkoa na jiji lenye rasilimali nyingi kama Dar es Salaam linakuwa na upungufu mkubwa kiasi hicho, basi kuna sababu zaidi za kuwa na wasiwasi kuhusu elimu kwa watoto walio katika wilaya zisizokuwa na rasilimali nyingi,” ilisema taarifa hiyo iliyotolewa na Mtendaji wa Twaweza, Rakesh Rajani.


Utafiti huo unaonesha kuwa pamoja na kuwapo karibu na ofisi zinazotunga sera, shule za msingi za Serikali jijini Dar es Salaam zina upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, madawati na vitabu.


Watafiti wamegundua kwamba wastani katika shule zote zilizotembelewa, wanafunzi watano wanalazimika kutumia kitabu kimoja kwa madarasa ya chini (Darasa la kwanza hadi la nne) na wanafunzi sita wanatumia kitabu kimoja katika madarasa ya juu (Darasa la 5-7). Miongoni mwa shule za msingi zilizotajwa, Kunduchi ambayo wanafunzi 10 wanatumia kitabu kimoja, Tandika wanafunzi 15 wanatumia kitabu kimoja.


Katika shule ya msingi Mbagala, utafiti umebaini kwenye madarasa ya juu walimu pekee ndio wana vitabu. “Zipo shule chache sana ambako chini ya wanafunzi watano wanatumia kitabu kimoja na mara nyingi ni kutokana na juhudi za wazazi wanaowanunulia watoto wao vitabu,” utafiti umebainisha.


Kuhusu msongamano madarasani, utafiti umebaini wastani wanafunzi 81 wanakaa kwenye darasa ambalo kwa kawaida linatakiwa kuwa na wanafunzi 40.


Vile vile karibu nusu ya shule zilizofanyiwa utafiti, wanafunzi wanakaa sakafuni kwa kuwa hakuna madawati ya kutosha.

Watafiti hao wamehoji zinakokwenda fedha ikizingatiwa kwamba kwa miaka ya karibuni, bajeti ya elimu imekuwa ikiongezeka.