RAIS Jakaya Kikwete amesema uongozi wake hauna muda tena wa kupoteza katika kuhakikisha kuwa wakulima wa Tanzania wanainuliwa kutoka kwenye umasikini.

Alisema atafanya hivyo kwa kuhakikisha kuwa kilimo cha Tanzania kinaboreshwa haraka

iwezekanavyo.

“Wangu ni uongozi usiokuwa na muda wa kupoteza. Nina haraka. Sina muda tena wa kusubiri. Tunahitaji kuongeza kasi ya mapambano ya kuwatoa wakulima wetu katika umasikini.


“Watu wetu wameishi katika umasikini kwa miaka mingi kupita

kiasi. Watu wetu wameteseka sana,” alisema Rais Kikwete juzimjini hapa.

Rais Kikwete aliyasema hayo wakati anashiriki katika kikao maalumu cha kujadili jinsi ya

kuanzisha Soko la Mazao la Tanzania ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa 21 wa Uchumi Duniani, Kanda ya Afrika, unaofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha mjini Cape Town, Afrika Kusini.

Mkutano huo ambao mwaka jana ulifanyika mjini Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza

kufanyika nje ya Jiji la Cape Town, umeanza jana mchana na mada kuu ya mkutano wa mwaka huu ni Nafasi ya Afrika katika Mazingira Halisi Mapya Duniani.

Akifunga kikao hicho juu ya uanzishwaji wa Soko la Mazao katika Tanzania, Rais Kikwete aliwaambia washiriki kuwa wakati umefika wa kukabiliana na umasikini ana kwa ana kwa nia ya kuupunguza na hatimaye kuumaliza kabisa kwa sababu wananchi wameishi katika maisha ya shida na dhiki kwa miaka mingi sana.


Washiriki wa kikao hicho walijadili uanzishwaji wa Soko hilo baada ya mawasilisho yaliyofanywa na Mtaalamu wa Masoko ya Mazao, Bharat Kulkarni ambaye ni

mchumi mkuu wa Soko la Mazao la Ethiopia.

Katika mawasilisho yake, Kulkarni ameeleza jinsi Soko la Mazao la Ethiopia alilosaidia

kuanzisha katika miaka ya karibuni linavyoshamiri.

Kulkarni pia ametoa maelezo ya jumla ya jinsi soko la mazao linavyotakiwa kufanya kazi, nani analimiki, nani analidhamini, nani anatoa fedha za uanzishwaji wake, nani wanashiriki katika shughuli zake, nani ananufaika nalo na kwa kiasi gani.