Ndugu zangu,


CCM inayumba, kusema kingine ni kuwadanganya CCM, haitawasaidia.
Ndio, jahazi linapopoteza mwelekeo kinachofuatia ni kuyumba na hatimaye kuzama. CCM kama chama, kiko hatarini kuzama. Kuna ishara zinazoonekana.

Nimeishi Iringa kwa miaka saba sasa. Nikiri, kuwa sijapata kushuhudia maandamano makubwa ya wafuasi wa chama cha siasa kama yale ya CHADEMA Alhamisi iliyopita. Sijapata pia kushuhudia mkutano mkubwa wa chama cha siasa kama ule wa CHADEMA pale viwanja vya Mlandege.


Na kuna Wana- CCM wenye kubeza; ” Ah, wale vijana wa CHADEMA ni wavuta bangi tu!” Ananiambia Mwana-CCM hapa Iringa. Nikamjibu; ” Kama vijana wale wa CHADEMA kwa mamia wameweza kujipanga vile wakaudhuria maandamano kwa amani na hata kukaa mkutanoni wakiwasikiliza viongozi wao, basi, bangi ya siku hizi inawatia watu akili kuliko kuwalewesha!”
Na si tuliona, pale Mlandege, kulikuwa na akina mama watu wazima pia. Katika Tanzania hii, ukiona mikutano ya Chama cha siasa inaanza kuhudhuriwa na akina mama watu wazima, basi, hicho si chama cha kukibeza.



Ndio, kwa CCM, CHADEMA sio wa kubezwa. Wahenga walinena; mdharau kipele hushtukia ana jipu. Unapoona wananchi wanaandama kwa miguu kwa kilomita 5 hilo si jambo la kubeza. Unapoona wananchi wanatoka Tanangozi, Ilula na kwengineko kwenda Iringa kumsikiliza Dr Slaa na wenzake, hilo si jambo la kubeza hata kidogo. Hapo kuna jambo.


Na kwa CCM, si busara kukimbilia kuwaparamia CHADEMA bali kuyafanyia kazi mengi ambayo CHADEMA wametumia majukwaa kuishtaki CCM na Serikali yake kwa Wananchi. Na katika hili, kuna Watanzania wanaiona CHADEMA kama wingu nene la mvua lililotanda angani kwenye nchi yenye ukame. Hata kama wingu litapotea bila mvua kunyesha, lakini bado , kwao ndio matumaini waliyo nayo, kwa sasa.



CCM haina jingine, bali kufanya kazi ya ziada kulinusuru jahazi lake lisije kuzama. Na Iringa ilikuwa moja ya ngome za CCM kisiasa, si hivi leo ninavyoandika. Kuna mawimbi makubwa wanayokwenda nayo CHADEMA kwa sasa, na kama fasheni, wengi wanaelekea kuyafuata mawimbi hayo. Na hata ukimwuliza mtu kwanini? Anakujibu; ” Chama ni CHADEMA tu!”.


Wenye kujibu hivyo hawajui ni kwanini hasa wanayafuata mawimbi hayo. Lakini wanajua walichokiacha nyuma yao, ni CCM. Kuna wanaosema wazi; ” Ah, CCM tumeichoka bwana!” Kwanini? Namwuliza jamaa wa mtaani; ” Tumeichoka tu, basi!” Na kuna wanaosema mitaani; ” CCM ni Chama Cha Mafisadi!”


Na hilo la mwisho ndio haswa ’ msalaba’ mzito waliojibebesha CCM, au labda wamebebeshwa. CCM ina lazima, sio tu ya kuutua msalaba huo, bali kuuchimbia shimo na kuuzika. Kwa namna gani? Si kwa kujivua gamba kama Chama, bali kuongoza juhudi za taifa zima kujivua gamba. Ndani yake kuna KATIBA MPYA, Miiko ya Uongozi, Kuheshimu Haki za Kibinadamu na mengineyo.


Maana, bila Taifa kujivua gamba, inaweza kesho ikaondoka CCM na wakaja CHADEMA. Kisha tukabaki tukisema; ” Alaa, tulistaajabia ya Mussa, tumeyaona ya Firauni!”


Na katika yote haya, CCM isije ikasahau dhamana yake kwa taifa. Ndio, CCM ni chama tawala. Ni chama kilichobeba dhamana kubwa ya uongozi wa nchi. Ni ukweli huo unaofanya yanayotokea ndani ya CCM yatuhusu sote hata tusio wafuasi wa itikadi za vyama.


Na historia ni mwalimu mzuri. Aliyekuwa kada wa CCM na Katibu Mkuu wa chama hicho marehemu Horrace Kolimba ndiye aliyeanza kuusema ukweli juu ya mwelekeo wa CCM. Ni zaidi ya miaka 20 iliyopita. Kolimba aliusema ukweli wake na akausimamia.


Alitamka hadharani, kuwa CCM imepoteza dira. Hata wakati huo, uongozi wa CCM uliikana kauli ya Kolimba. Kolimba alikuwa na ujasiri wa kuisimamia kauli yake hadi kufa kwake. Atakumbukwa daima kwa kauli na msimamo ule aliouonyesha.


Miaka mingi imepita tangu Kolimba atamke kauli ile. Tumeanza kusikia sauti nyingi zaidi zikitamka mambo yenye kufanana na yale aliyoyasema Kolimba. Alianza Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ikafika mahali Mwalimu hakuishia tu kuzungumza juu ya yanayotokea ndani ya chama chake. Mwalimu aliandika kitabu ili kuacha kumbukumbu ya kudumu juu ya alichotaka kusema.


Hata baada ya Mwalimu tumeanza kuwasikia makada wengine wa CCM wenye kutamka hadharani yale yenye kufanana na ya Kolimba na Mwalimu. Ni leo tu, tumesoma kauli ya Mzee Ibrahim Kaduma, kuwa CCM imepoteza mwelekeo.


Kwamba wana- CCM wenyewe wameanza kujihoji ni jambo la heri kwa chama hicho tawala. Wenye kuhoji yanayotokea ndani ya CCM wanafanya hivyo kwa mapenzi mema na chama chao, hata kama wanajiweka katika hatari ya kupigwa mihuri ya “upinzani’ na kuhatarisha kutengwa kutoka kwenye kundi kuu.


Tunapozungumzia dhana ya kuimarisha demokrasia ya ndani ya vyama ( Intra-party democracy) si jambo la busara hata kidogo kujaribu kuzuia sauti zenye kuhoji, kudadisi na hata kupinga na kushutumu. Si busara hata kama wenye kuhoji na kudadisi ni kumi tu kati ya wanachama milioni moja.


Hata katika familia ya watoto wa tumbo moja wote hawawezi kuwa na fikra na mitazamo yenye kufanana. Kuzizima sauti hizo kunasaidia tu kuongeza manung’uniko na minong’ono ya chini chini. Zinachangia kuongezeka kwa harakati za chini kwa chini.


Manung’uniko, minong’ono na makundi yanaimarika pale ambapo wenye fikra na mitazamo tofauti wanapobanwa sana ndani ya chama na hata kufikia kukosa majukwaa ya kusemea. Ni pale watu hao wanapojisikia hofu ya kuchapwa bakora za chama na hata kutengwa kutoka kwenye kundi kuu. Hofu hiyo hupelekea nidhamu ya woga na watu kutoaminiana. Hupalilia zaidi hulka za kinafiki.



Wanachohitaji CCM kwa sasa ni kurudi kwenye misingi yao iliyopelekea kuundwa kwa Chama mama TANU na Afro-Shiraz na baadaye kuzaliwa kwa CCM. CCM irejee kwenye misingi yake ya miiko na maadili ya uongozi. Na irejee kwenye ahadi za mwanachama wa chama hicho kwa chama chake. Moja ya ahadi muhimu za mwana TANU na baadaye Mwana – CCM ni hii ifuatayo; ” Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko”.


Nakumbuka, Tambwe Hizza, aliyeingia CCM akitokea CUF alipata kutamka hadharani, kuwa walipokuwa upinzani kazi yao ilikuwa ni kutunga uongo. Alichomaanisha Tambwe Hizza ni kuwa kama alikuwa ni mmoja wa watunga uongo kwenye kambi ya upinzani, basi, kuondoka kwake kutoka upinzani na kujiunga na CCM kulikuwa ni jambo la heri kwa aliowaacha huko kwenye upinzani. Bila shaka waliobaki huko walifurahia kwa kuondokewa na mtu mwongo.


Imefika wakati kwa Wana-CCM kuacha hofu ya kuambizana ukweli. Tulio nje tunakiona chama kinachoyumba. Rushwa na ufisadi ndani ya chama zinakiyumbisha chama. Ndani ya CCM kuna wanaoliona hilo pia. Baadhi yao kwa unafiki watamwambia nahodha; “Kanyaga mafuta baba!” Huku wakijua kinakoelekea chombo siko.


Na kila jahazi huwa na panya wake. Wenye kumsisitiza nahodha akanyage mafuta mara nyingi huwa na tabia za panya wa jahazini. Jahazi likianza kuzama, panya wake huwa wa kwanza kurukia majini na kukiacha chombo kikizama.


Inahusu umuhimu wa kusema yaliyo ya kweli. Na kuna aina tatu za wasema kweli. Kuna anayeusema ukweli na kujificha. Huyu anaweza kuwa na sababu za msingi za kutaka kuusema ukweli na kujificha. Ndiyo huyu atakayekwambia ukweli juu ya jambo fulani kisha kukutamkia; ”Tafadhali jina langu lihifadhi”.


Aina ya pili ya msema ukweli ni yule anayeusema ukweli na kisha kuukimbia. Atausema ukweli, akibanwa sana na wenzake, basi, ghafla ataukanusha ukweli aliousema hadharani. Atauruka ukweli wake mwenyewe. Atayakanusha maneno yake hata kama yamerikodiwa kwenye kaseti na kila mmoja akayasikia. Atang’aka, atakikimbia kivuli chake. Hii inatokana na woga unaozaa unafiki.


Lakini mwisho, kuna huyu anayeusema ukweli na kisha kuusimamia kwa lolote lile. Inyeshe mvua liwake jua. Ni watu wa aina ya akina Kolimba. Jamii yetu ilihitaji kuwa na watu wengi zaidi wenye kulikaribia kundi hili la tatu la wasema ukweli. Na siku zote , ukweli ni mzigo mzito, haupaswi kubebwa. Ukweli husambazwa.


Maggid,