SERIKALI ya China imetoa msaada wa Sh milioni 375 kwa Jeshi la Polisi ili kusaidia ununuzi wa mahitaji muhimu kwa ajili ya kuimarisha utendaji wa Jeshi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi jana Dar es Salaam, hati za msaada huo zilisainiwa na Waziri Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Waziri wa Wizara ya Usalama wa Raia wa China, Zhang Xinfeng aliyepo nchini kwa ziara ya siku tano.
Ilielezwa katika hafla hiyo, Vuai alisema misaada hiyo itatumika kwa usahihi ili kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaimarishwa.
Aidha, kwa upande wake Zhang alisema Serikali ya China itaendelea kulisaidia Jeshi hilo katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafunzo ndani ya nchi na nchini China pamoja na vifaa muhimu vinavyohitajika katika kulinda usalama na utulivu.
Kwa mujibu wa Zhang, China na Tanzania zimekuwa marafiki wa muda mrefu ambapo ni muhimu kwa serikali hizo kuhakikisha ushirikiano uliopo hasa katika suala la usalama wa raia unaimarishwa.
Kabla ya kusaini hati hizo, Vuai alisema kuimarishwa kwa ulinzi na usalama wa raia na mali zao nchini kunakwenda pamoja na kuhakikisha mali za wawekezaji kutoka nje ikiwemo China zinalindwa.
Zhang alisema pamoja na maendeleo ya kiuchumi yanayotokea kwao, wanakabiliwa na changamoto nyingi juu ya usalama wa umma na ili kukabiliana nazo ni muhimu kuimarisha uwezo wa vyombo vya ulinzi na usalama wa raia wa nchi hizo mbili.
0 Comments