Waasi wa Libya wanasema wameuteka uwanja wa ndege wa mji wa Misrata, na kuwatimua wanajeshi wa Kanali Muammar Gaddafi.
Mamia ya waasi walikuwa wanasherehekea katika barabara za mji huo,baada ya vikosi vinavyomuunga mkono Gaddafi kukimbia, na kuacha vifaru vya kijeshi ambavyo vilichomwa moto,mmoja wa walioshuhudia alisema.

Vikosi vya serikali vimekuwa vikishambulia mji huo wa magharibi,ambao kwa sehemu kubwa unadhibitiwa na waasi.
Wakati huo huo,kituo cha televisheni ya kitaifa cha Libya kimeonyesha video ya Kanali Gaddafi akiwa kwenye mkutano na viongozi wa makabila mbali mbali katika mji mkuu wa Tripoli.

Video hiyo ilichukuliwa Jumatano jioni,afisa mmoja wa Libya aliambia shirika la habari la AFP.Taarifa hizi hazijaweza kuthibitishwa.
Kanali Gaddafi hajaonekana hadharani tangu tarehe 30 mwezi uliopita - wakati shambulio la ndege ya Nato lilipomuua mwanawe wa kiume,mwenye umri wa miaka 29 Saif al-Arab, na wajukuu zake watatu.
Kumekuwa na taarifa za mashambulio mengine katika mji mkuu wa Tripoli siku ya Jumatano.