Serikali ya Libya imesema imewaachia huru waandishi wa habari wa kigeni wanne waliotiwa kizuizini kwa kuingia nchini humo kinyume cha sheria.
Waandishi wa habari wawili wa Marekani na mpiga picha kutoka Hispania wameachiwa.
Kulikuwa na mkanganyiko wa utambulisho wa mwandishi wa habari wa nne na hatima ya mpiga picha wa Afrika kusini haijajulikana.
Msemaji wa serikali Moussa Ibrahim alisema wale walioachiwa wanaweza kubaki na kuendelea na kazi zao nchini humo.

Serikali ya Libya imekuwa ikipambana tangu mwezi Februari.
Wamarekani walioachiwa huru ni James Foley wa GlobalPost na mwandishi wa kujitegema Clare Morgana Gillis. Na raia wa Hispania ni Manu Brabo.
Wa nne aliyachiwa ametajwa na mashirika ya habari kuwa ni Mwingereza Nigel Chandler.
Hakuna mwenye jina hilo ameripotiwa kuwa hajulikani alipo, japo mwandishi wa habari wa Uingereza aitwaye Nigel Taylor aliripotiwa kutojulikana alipo tangu mwezi Machi.
Bi Gillis ameliambia shirika la habari la AP kuwa wote wanne walikuwa kwenye hoteli ya Rixos mjini Tripoli na walikuwa wakiendelea vizuri.
Hatima ya mpiga picha wa Afrika kusini, Anton Hammerl, aliyeshikiliwa Aprili 4, bado haikuwa wazi.