Amnesty International inasema kwamba machafuko ya baada ya uchaguzi yamewaacha raia wa Ivory Coast na mafadhaiko makubwa, kwenye ripoti yake ya kina ambayo imesema taifa hilo lilishuhudia machafuko mabaya zaidi tangu kugawanyika mara mbili hapo mwaka 2002.
Watatifiti wa ripoti hiyo waliwahoji mashahidi waliopoteza jamaa zao katika ghasia zilizolenga makabila pamoja na waathirika wa ubakaji uhalifu unaolaumiwa kutekelezwa na pande zote.

Takriban watu elfu tatu walipoteza maisha katika machafuko hayo huku maelfu wakikimbia makaazi yao, baada ya rais Laurent Gbabgo, kukataa kuridhia kushindwa katika uchaguzi wa urais mwaka jana.
Machafuko mabaya zaidi yalitokea katika mji wa Duekoue,ambapo mamia ya raia waliuawa baada ya eneo hilo kutwaaliwa na wanajeshi watiifu kwa rais mteule Alassane Ouattara.
Kiongozi huyo ameahidi kuhakikisha pande zote zinachunguzwa ambapo amemuomba mwendesha mashtaka mkuu katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita kuchunguza uhalifu wa kivita nchini humo.
Ripoti hiyo ya Amnesty International, aidha imelaumu vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa ikisema vilikosa kuzuia mauaji katika mji wa Duekoue ambao uko karibu sana na kambi walinda amani hao.
Wengi wa raia waliolengwa ni kutoka jamii ya Guere waliopigwa risasi na wanawake kubakwa.
Hata hivyo maafisa wa Umoja wa Mataifa mjini Abidjan, wamesema hawakupokea ujumbe wowote kukiimarisha kikosi chake katika eneo hilo ili kukabiliana na machafuko yaliyokuwa yakiendelea.
Wakati mahakama ya ICC ikianza uchunguzi wake nchini Ivory Coast, mwendesha mkuu wa mashataka nchini humo naye ameanzisha uchunguzi wake wakati huku tume ya haki na maridhiano ikitarajiwa kutangazwa.