Wakristo katika mji mkuu wa Misri, Cairo wanafanya sala maalum karibu na eneo la wazi la Tahrir Square kufuatia shambulio katika makanisa mawili lililoua watu kumi na wawili.
Zaidi ya watu 180 walijeruhiwa katika mapigano Jumamosi baada ya waislamu wenye msimamo mkali kushambulia kanisa katika eneo la Imbaba.
Waandamanaji wamekusanyika nje ya kituo cha televisheni ya Taifa wakilishutumu jeshi la nchi hiyo kushindwa kuwalinda.

Jeshi la Misri linasema zaidi ya watu 190 wamekamatwa baada ya ghasia hizo na kuwa watashtakiwa katika mahakama za kijeshi.
Baraza la kijeshi linaloongoza nchi hiyo kwa sasa limesema hatua hiyo ni kuzuia ghasia nyingine zaidi.
Waziri wa sheria Abdel Aziz al-Gindi ameonya kuwa wanaotishia usalama wa nchi watapambana na mkono wa chuma'.
Waziri huyo alizungumza baada ya kikao cha dharura cha mawaziri kilichoitishwa na waziri mkuu Essam Sharaf aliyearisha ziara yake nchi za Ghuba.

Bwana Gindi alisema serikali 'itaanza mara moja kutekeleza sheria zinazohusu uhalifu wa mashambulizi dhidi ya nyumba za ibada na uhuru wa kuabudu,' ambazo zitaruhusu hukumu ya kifo kutumika.
Machafuko ya Jumamosi yalianza baada ya mamia kadhaa ya waislamu wenye msimamo mkali wa kikundi cha Salafist kukusanyika mbele ya kanisa moja katika wilaya ya Imbaba.