Mwenyekiti wa Chama cha (UPDP), Fahmi Dovutwa(Pichani kushoto mwenye kofia), amemshauri Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, kuwa na utaratibu wa kuwapima akili wagombea wa vyama mbalimbali kabla ya kupewa fursa ya kugombea nafasi za kisiasa.
Amesema wanasiasa wengi nchini ndio wamekuwa vyanzo vya vurugu, uchochezi wa kuvunja amani ya nchi, na kuweka utashi wa maslahi yao wenyewe badala ya kuelimisha wananchi haki na wajibu wao.
Dovutwa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipowakilisha viongozi wa vyama vya siasa nchini katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu ziara ya utalii ya Balozi wa Amani wa Universal Peace Federation (UPF), Risasi Mwaulanga.
Aliongeza kuwa wanasiasa wapimwe akili zao kutokana na mambo wanayoyafanya kuwa kinyume na taratibu za uongozi kwani wanatakiwa wawe wazalendo na watumie haiba walizonazo kwa kuwaelimisha wananchi katika masuala mbalimbali, likiwemo la kutembelea vivutio vya ndani ya nchi ili kukuza pato la nchi.
"Kama sera ya utalii nchini inavyojieleza kuwa jukumu la kuutangaza utalii na kuendeleza ni la kila Mtanzania, wanasiasa na vyama vyao wanawajibu usiokwepeka katika suala zima la kutangaza na kuendeleza vivutio na maliasili zetu za nchi," alisema Dovutwa.
Alisema wanasiasa ni sehemu ya Watanzania wengi ambao wapo katika lindi la usingizi na kukosa ufahamu kwa kuamini utalii ni maalum kwa wageni tu kitu ambacho kimezorotesha idadi ya watalii wa Kitanzania katika hifadhi za nchini.
Naye Balozi huyo wa Amani wa UPF, alisema katika ziara yake aliyoifanya Mei 8, mwaka huu katika Hifadhi za Tarangire na Manyara mkoani Arusha pamoja na Ngorongoro, aliona kasoro ambazo zinapaswa kurekebishwa kama ukosefu wa matangazo mengi na juhudi za kizalendo, ujangili na uvunaji ovyo wa rasilimali hasa misitu na nyuki.
Kasoro nyingine alisema ni kutotumia vizuri fursa zinazojitokeza kutokana na haiba ya Rais Jakaya Kikwete kukubalika katika Jumuiya za Kimataifa ikiwemo ya wanasiasa na wafanyabiashara hivyo wadau wa sekta ya utalii watumie fursa hizo kukuza pato la taifa kupitia vivutio vilivyopo.
0 Comments