KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama amewataka wanachama wa chama hicho wilayani Tarime kuwa na mshikamano na kutotoa siri za vikao vya chama.
Akizungumza katika kikao cha ndani cha chama hicho juzi, Mukama alisema, wapinzani hawana hoja bali wanasubiri hoja za CCM, hali inayoleta mgongano ndani ya wanachama wao.
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere, Katibu Mkuu UWT Taifa, Amina Makiragi na Katibu wa CCM Mkoa, Ndekubali Ndengaso, Mukama alisema CCM imefanya mageuzi ndani ya ngazi za juu.
Kuhusu mageuzi hayo, Mukama alisema aliyekuwa Katibu Mkuu, Yusuf Makamba na Kamati Kuu walijiuzulu kwa nia ya kuimarisha chama upya.
Aliwataka viongozi na wanachama wa CCM wajitume kufanya kazi kuanzia ngazi za mashina ikiwemo kufanya vikao vya mara kwa mara na wanachama, ili kuvuna wanachama wapya kutoka vyama vya upinzani.
"Wapinzani hawana hoja , wanazitafuta kutoka kwa wanachama wa CCM ambao hawafuati maadili ya chama, waache watafute na kuibua hoja zao wenyewe kutoka ndani ya vyama vyao ili wananchi wawatafakari wanayoyasema kama ni ya kweli ama uongo,” alisema.
Alielezea kusikitishwa na maafa yaliyowakumba vijana watano wanaodaiwa kujaribu kuvamia mgodi wa North Mara Barrick uliopo Nyamongo na kulaani vyama vya siasa vinavyotumia vibaya msiba huo.
Pia alilaani vyama vinavyowachochea vijana kuvamia mgodi na kufanya uhalifu na matokeo yake ni maafa kama hayo yaliyotokea.
Akiwa katika Wilaya ya Rorya, Mukama aliweka jiwe la msingi katika Ofisi ya CCM Kata ya Bukwe na kuchangia Sh milioni 2 katika ujenzi huo ambao jengo limefikia katika lenta.
0 Comments