JESHI la Polisi mkoani Rukwa linamtafuta mwanamke mmoja mkazi wa mtaa wa Lwiche Kitongoji cha Mazwi katika Manispaa ya Sumbawanga kwa tuhuma ya kumchoma sindano iliyowekwa maji ya moto mtoto mwenye umri wa miaka sita kwenye sehemu yake ya haja kubwa kwa madai kuwa ni kikojozi.

Mwanamke huyo aitwaye Severia Mpepo anatuhumiwa kumfanyia unyama huo mtoto huyo na kumsababishia maumivu makali juzi majira ya saa moja asubuhi.



Kitendo hicho kisicho kawaida kilisababisha mtoto huyo ambaye ni wa kiume kupiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa majirani kabla ya kuzimia na kukimbizwa na wasamaria katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa kwa ajili ya matibabu.


Kwa mujibu wa majirani wa mtoto huyo ambao hawakutaka kutajwa majina yao walisema kuwa tukio la kuunguzwa linafuatia mateso mfululizo aliyokuwa akiyapata kutoka kwa mama mlezi wake, Severia ambaye amekuwa akimlea kwa kipindi cha miezi sita tangu kufariki kwa mama mzazi wa mtoto huyo.


Majirani hao walisema mtoto huyo aliletwa kwa mlezi huyo na babake mzazi anayefahamika kwa jina la Peter Matalanganya kufuatia ushauri wa rafiki yake ambaye ndiye mume wa Severia aliyemshauri kuwa ampeleke kwake ili apate kumlea baada ya mkewe kufariki dunia.


“Tunasikia kuwa huyu mtoto aliletwa hapa na babake miezi sita iliyopita baada ya mamake kufariki, lakini kuanzia alipofika huyu mwanamke amekuwa akimtesa sana mara amnyime chakula, mara amchape na juzi ndio kahitimisha kwa kumfanyia huu unyama wa kumwunguza katika sehemu yake ya haja kubwa, kwa kweli huyu mama hafai na ni muuaji mkubwa,“ walisema majirani hao.


Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Saduni Kabuma alikiri kumpokea mtoto huyo hospitalini hapo na kupatiwa tiba ambapo katika uchunguzi alionekana kuwa ameunguzwa katika sehemu za haja kubwa na maji hayo kiasi cha kumsababishia malengelenge.


Dk. Kabuma alisema kuwa taarifa alizopata kutoka kwa ndugu wa karibu waliomfikisha hospitalini hapo zimedai mama mlezi wa mtoto huyo alichukua uamuzi huo wa kinyama kwa kuwa kijana ni kikojozi wa kupindukia.


Naye Daktari aliyempokea mtoto na kumpatia huduma ya matibabu katika kitengo wagonjwa wa nje, Dk. Revocatus Kasoni alisema kuwa hali ya mtoto huyo inaendelea vizuri na kuongeza kuwa bado yupo katika uchunguzi wa kitabibu zaidi.


Alipoulizwa na waandishi wa habari waliofika nyumbani kwake kutaka kufahamu undani wa tukio hilo alikiri kutenda unyama huo, lakini alisema hakutenda kwa makusudi bali alikuwa anampatia mtoto huyo tiba ya ugonjwa wa tumbo kwa kumpiga bomba.


Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa Isuto Mantage alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema kuwa mama huyo bado hajakamatwa na Jeshi hilo linaendelea kumsaka mama huyo ili sheria ichukue mkono wake iwapo ikibainika kuwa alitenda uovu huo.


(Source Habari Leo).