FAMILIA ya aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu hayati Rashidi Kawawa, imesema itapigania kulinda heshima ya mwanasiasa huyo baada ya kuwapo tishio la nyumba yao iliyopo Kilimani mjini Dodoma inauzwa na kupangishwa na mama yao wa kambo. (Pichani ni Zainab Kawawa mtoto wa marehemu mzee Kawawa)
Mama huyo, Asina Kawawa, anadai kuwa nyumba hiyo ni mali yake. 

Kwa mujibu wa familia hiyo, nyumba hiyo inataka kupangishwa na mama huyo anayedai kwamba alirithishwa na Kawawa, licha ya familia kueleza kutotambua hilo, lakini pia ni makumbusho na moja ya maeneo ya kihistoria ya mwanasiasa huyo aliyepigania Uhuru wa Tanganyika.


Ingawa mama huyo anadaiwa kuwa mbioni kupangisha nyumba hiyo iliyopo kiwanja namba 34 eneo la Uzunguni mjini hapa, lakini ipo hatarini kuuzwa na benki ya CRDB baada ya kutumika kama dhamana ya mkopo wa Sh milioni 350 kwa ajili ya kujenga nyumba nyingine pembeni mwa hiyo, mali ya Asina.


Mmoja wa wanafamilia ya Kawawa, Zainab Kawawa ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), aliwaeleza waandishi wa habari akiwa katika nyumba hiyo, kwamba familia inataka kulinda na kutunza heshima ya Mzee Kawawa, kwa sababu hakuwa mtu wa kukopakopa ovyo.

“Tunataka kulinda heshima ya Mzee Kawawa, tumemweleza mama kuwa tuko tayari kulipa deni hilo, lakini hayuko tayari, kwa sababu anaamini tukilipa deni nyumba hii itakuwa yetu, lakini zaidi ni kwamba tayari kuna notisi ya CRDB ya kuuza nyumba kutokana na deni,” alisema Zainab.
Alisema licha ya kuomba mkopo wa Sh milioni 350, ambao ulikuwa ukitolewa kwa awamu, mama huyo alipewa Sh milioni 74 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba hiyo ya ghorofa moja nyuma ya nyumba ya Mzee Kawawa, lakini sasa deni hilo limefikia Sh milioni 102.

“Kama familia, tulikaa na kuzungumzia deni hili na kukubaliana kuwa linatuhusu, hivyo baadaye lilisimamishwa na sasa limefikia Sh milioni 102, na tayari CRDB wanataka kuja kuuza nyumba hii kwa sababu ya deni,” alisema Zainab ambaye alizungumza na wanahabari baada ya mkutano kati yake na mama yake na mwanasheria Ngonyani kutoka makao makuu ya CCM.


Alisema kwa mujibu wa maelezo ya mama yao, nyumba hiyo aliyokuwa akiishi Mzee Kawawa kwa muda mrefu, aliinunua kwa ubia mwaka 2007 kutoka serikalini na inadaiwa kuwa ilikuwa na kipengele cha kuwa mmojawapo akifariki dunia, basi anayebaki atairithi.


“Tulisimamisha mkopo huo kama familia na tunaendelea sasa kuulipa, na tulizungumza na mama namna ya kulipa. Kwa masharti kwamba tulipe deni na kisha tumwachie eneo analojenga, aendelee nalo na sisi tubaki na hii nyumba, na hili linafanyika sasa kwa watu wa Ardhi, lakini mama halitaki, anang’ang’ania nyumba na sasa analeta mpangaji,” alisema Zainab na kuongeza:


“Hatushindwi sisi kulipa deni hili, na ndiyo maana tumekubaliana kulipa, lakini tunachotaka ni kulinda heshima ya Mzee Kawawa. Baba hakuwa mtu wa kukopakopa mamilioni benki. Na hivi benki inamkopeshaje mtu ambaye alishavuka wastani wa umri wa kuishi. Ninyi hamwoni ajabu?”


Alisema mama yao huyo aliyeolewa mwanzoni mwa miaka ya 2000, hana uwezo wa kulipa deni hilo na hasa ikizingatiwa kila mwezi inatakiwa kulipiwa Sh milioni nane, na kuhoji hata kama atapangisha mtu, atampangisha kwa kiasi gani kufidia deni hilo.


“Si kweli kwamba sisi tunaitaka nyumba hii, lakini tunaitaka kwa sababu baba aliishi hapa na mama yetu wa kwanza, wa pili na wa tatu (Asina) na kila mmoja anajua nyumbani hapa na panatambulika kama Uzunguni kwa Kawawa. Sasa iweje leo, tuache eneo la historia ya baba lichafuliwe, heshima yake idhalilishwe. Hatuko tayari kuona hapa panauzwa,” alieleza Zainab.


Alisema baba yao aliyefariki dunia Desemba 31, 2009 alikuwa mtu aliyejipanga vyema, kwani aliwaacha kila mtoto ana nyumba kupitia kwa mama zao, na kudai kuwa hata mama yao huyo ana nyumba mbili, Mbweni Dar es Salaam na Tabora alizojengewa na Mzee Kawawa na mali nyingine.

Kuhusu mirathi, alisema mama yao amekataa suala hilo na ndiyo maana wamefikia hali hiyo, huku akimtuhumu mama yao, kwa kuivuruga familia na kusababisha matatizo yote hayo.

Mama Asina kwa upande wake, alisema nyumba hiyo aliipata kihalali baada ya kununuliwa na mumewe kutoka serikalini mwaka 2007, na kwamba aliandikishwa urithi yeye; ndio sababu ni mali yake.


“Waandishi hii ni mali yangu na hata kwenye fomu za kununua (akiwaonesha baadhi ya waandishi), nimeandikwa jina langu na wanunuzi wawili, mimi na Mzee Kawawa,” alifafanua mama huyo.


Akiwa amefuatana na ndugu zake kadhaa akiwamo aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Abdallah Zombe, Mama Asina alisema alikwenda na mwanasheria huyo kwa ajili ya kufanya tathmini na alimwagiza kuendelea na kazi hiyo kwa sababu Zainab si mali yake.


Zombe akizungumza katika kikao hicho, aliomba familia hiyo ya mmoja wa wanasiasa wazalendo wa Tanzania, kutumia fursa ya vikao kumaliza kadhia hiyo, ambayo ilionekana dhahiri itachafua jina safi la Simba wa Vita na hasa baada ya kutokea kurushiana maneno makali kati ya mama na Zainab.


Baadhi ya viongozi wa serikali wa mkoa wa Dodoma, walifika nyumbani hapo jana asubuhi baada ya mzozo kati ya mbunge huyo na mama yake, katika kile kinachoaminika ni kujaribu kusawazisha mambo.