Ongezeko la bei za vyakula litawaathiri watu maskini zaidi ambao tayari wanahangaika kununua chakula cha kutosha, wakitaka mabadiliko makubwa kwa mfumo mzima wa chakula duniani, Shirika la Oxfam limeonya.
Inakadiriwa kuwa mpaka mwaka 2030 bei ya wastani ya mazao muhimu itapanda kwa asilimia 120 hadi 180, kwa mujibu wa makadirio ya wahisani.
Huu ni mwendelezo wa hali ambayo tayari imeshuhudiwa ya kupanda kwa bei za vyakula mara mbili katika kipindi cha miaka 20.
Nusu ya ongezeko lijalo la bei za vyakula litakuwa ni kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, Oxfam limetabiri.
Limetoa wito kwa viongozi wa dunia kupitia upya mfumo wa masoko ya vyakula na kuwekeza fedha zaidi katika mfuko wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani.
"Mfumo wa vyakula lazima upitiwe upya iwapo tunataka kukabiliana na changamoto zinazooongezeka za hali ya hewa, ongezeko la bei za vyakula na upungufu wa ardhi ya kutosha, maji na nishati” alisema Barbara Stoking, Afisa Mtendaji wa Oxfam.
Bei za vyakula tayari zilishapanda zaidi ya mara mbili tangu 1990, kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), na Oxfam linatabiri kuwa hali hii itaendelea kuongezeka kwa miaka 20 ijayo.
Katika taarifa yake, Oxfam linasema makadirio yanaonyesha kuwa idadi ya watu duniani itafikia bilioni tisa ifikapo mwaka 2050 lakini wastani wa mazao ya kilimo ulishapungua kwa karibu nusu tangu mwaka 1990.
0 Comments