MBUNGE wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema), ameishinikiza Serikali kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri ili kuokoa fedha za umma.

Katika hatua nyingine, Bunge limeshinikizwa kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuhamishia ofisi yake Dodoma kama mkakati wa kuhamishia Makao Makuu ya Serikali mjini hapa.


Lyimo aliwasilisha hoja hiyo bungeni jana alipokuwa akichangia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyoiwasilisha bungeni Alhamisi iliyopita.


Mbunge huyo alisema ukubwa wa Baraza la Mawaziri la Tanzania umezidi hata mataifa makubwa duniani kama Marekani, China, Japan na Ujerumani kutokana na Baraza hilo kuwa na mawaziri 52.


Alisema Marekani inayoongoza kiuchumi duniani ina mawaziri 15 tu, Japan iliyopo nafasi ya tatu kwa ubora wa uchumi duniani ina mawaziri 17, wakati Ujerumani ambayo inashika nafasi ya nne kwa uchumi wa dunia ina mawaziri 15 tu pia.


“Mheshimiwa Spika inashangaza sana kuona nchi kama Tanzania yenye uchumi wa asilimia saba tu inakuwa na Baraza la Mawaziri kubwa mara tatu kupita Marekani, hii inasababisha uharibifu wa fedha za umma na kuliongezea Taifa umasikini,” alisema Lyimo.


Akizungumzia kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Dodoma, alisema mpango huo ni kama kiinimacho kwa Watanzania kwani badala ya kutenga fedha za ujenzi wa Ofisi za Serikali Dodoma, fedha zimekuwa zikitengwa kujenga na kukarabati ofisi zilizopo Dar es Salaam.


Alisema ingawa kuna ushauri kwamba Spika wa Bunge, ahamie Dodoma ili na ofisi nyingine za Serikali ziige mfano huo, lakini ni vema kama Rais atakuwa wa kwanza kuhamia Dodoma na kufuatiwa na Waziri Mkuu kwa vile ndiyo watendaji wakuu wa shughuli za Serikali.


“Mimi sidhani kama Spika ni muhimu sana kuanzisha mchakato huu wa kuhamia Dodoma, ni vema kama ataanza Rais mwenyewe na Waziri Mkuu. Wakifanya hivyo wao sidhani kama kuna kiongozi atabakia Dar es Salaam, lakini vinginevyo hilo halitafanikiwa,” alisema.


Mbunge huyo pia alizungumzia kuhusu migomo kwenye vyuo vikuu akisema unatokana na Serikali kushindwa kushughulikia kero na matatizo ya wanafunzi hao kikamilifu. (Habari Leo).