KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeliagiza Jiji la Tanga kuikabidhi kamati hiyo nyaraka zinazoonesha mchakato wa kumrejesha kazini Ofisa Ardhi wa Jiji hilo baada ya kufukuzwa kutokana na tuhuma za kuuza viwanja zaidi ya mara mbili na kusababisha hasara.


Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Agustino Mrema imetoa agizo hilo kutokana na taarifa za Jiji hilo kwamba ofisa huyo, Makwasa Biswalo amerejeshwa kazini licha ya kufukuzwa na Jiji hilo na adhabu yake kuthibitishwa na Tume ya Utumishi wa Umma.


Katika taarifa yake kwa kamati, Mkurugenzi wa Jiji, Gikene Mahene alisema Biswalo alifukuzwa baada ya kutuhumiwa kuuza zaidi ya viwanja 70 na kila kimoja kuuzwa kwa mtu zaidi ya mmoja na kusababisha migogoro.


“Baada ya kuibuka migogoro mara kwa mara tulifanya uchunguzi na kubaini Biswalo alikuwa akitoa kiwanja kimoja kwa watu zaidi ya wawili ambapo katika moja ya kesi Jiji lililazimika kulipa Sh mil 3.5 kwa mmoja wa wananchi aliyeuziwa kiwanja” alisema.


Mahene alisema baada ya mchakato wa kumfukuza kazi, mtumishi huyo alikata rufaa katika Tume ya Rais ambayo pamoja na Jiji na Tume ya Utumishi kuthibitisha makosa yake waliamua kumrejesha kazini.


Mrema pamoja na wajumbe wengine wa kamati hiyo Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Kiwanga, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi na Mbunge wa Kondoa Kaskazini, Zabein Mhita walimtaka mtumishi huyo kurejesha fedha zilizolipwa.


Walisema, mtumishi huyo amelisababishia hasara jiji hilo ni vyema akarejesha fedha ambazo zimelipwa kwa wananchi waliouziwa viwanja zaidi ya mara mbili lakini pia Kamati ipewe mchakato wa jinsi alivyorejeshwa kazini.


“Mimi siamini kama Rais Jakaya Kikwete anaweza kuridhia watumishi wazembe kurejeshwa kazini…hebu tuleteeni hizo barua hapa sisi tutaenda kuhoji hizo mamlaka sababu za msingi za kumrejesha kazini” alisema Mrema.


Kamati hiyo ilisema haiwezi kuridhia uamuzi huo kwani kwa kufanya hivyo ni kuisababisha Serikali hasara zinazoweza kuepukika
.