MTUHUMIWA wa ujambazi aliyekuwa amevaa sare za Polisi ameuawa na mwili wake kuteketezwa kwa moto katika eneo la Jangwani, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.

Mtu huyo ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja anayekadiriwa umri wa kati ya miaka 20 na 23, aliuawa wakati alipokuwa kwenye harakati za kuvunja na kuiba katika eneo la Jangwani mjini hapa akiwa na wenzake ambao pia ilielezwa walikuwa na sare za Polisi.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage alisema tukio hilo ni la juzi saa 9 alfajiri .


Alisema watu hao walivamia nyumbani kwa Faraji Said 'Mkikima' na kuvunja mlango wa geti nakuingia ndani.


“Ndipo marehemu alipokwenda na kupitia kwenye tundu lililopo kati ya paa na mlango wa sebuleni kwa lengo la kuwafungulia wenzake ...ghafla mwenye nyumba alishtuka na kuanza

kupiga kelele ambapo wananchi wengi walijitokea na kuanza kumshambulia hadi akapoteza fahamu na kama vile haitoshi mwili wake wakauteketeza kwa moto. Wenzake walikimbia ,” alisema.

Kwa mujibu wa Kamanda, uchunguzi wa awali ulibaini kuwa kabla ya tukio hilo, mtu huyo

aliyeuawa na wenzake wakiwa wamevaa makoti marefu yanayofanana na sare za Polisi nchini, walimvamia mwananchi na kumnyang'anya Sh 90,000- na simu ya mkononi.

Inadaiwa kuwa mtu huyo alifika kituo cha Polisi mjini Sumbawanga akilalamika kuwa

amevamiwa na askari Polisi ambaye alimnyang'anya mali zake.

Polisi inaendelea na uchunguzi na hakuna aliyekamatwa kwa mauaji ya mtuhumiwa
.