Wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakimpongeza Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, mara baada ya Mahakama ya Hakimu Mkuu Mkazi Mkoa wa Arusha kumuachia kwa dhamana mwanasiasa huyo anayekabiliwa na kesi ya kushirikiana na wenzake wakiwemo wabunge kuandaa mkutano na kuandamana kinyume cha sheria. (Picha na Marc Nkwame).
KUKAMATWA kwa Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, kulisababishwa na mdhamini wake.
Julius Margwe ambaye jana alikataliwa na Mahakama ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Mkoa wa Arusha kuendelea kumdhamini Mbowe, alikiuka masharti ya Mahakama kwa kutofika mahakamani kumwakilisha mdhaminiwa ambaye naye hakuwapo Mei 27.
Hakimu Charles Magesa badala yake jana alimkubali John Bayo ambaye ni Diwani wa Elerai mkoani Arusha kuwa mdhamini mpya wa Mbowe.
Mbowe aliachiwa jana kwa dhamana baada ya kusafirishwa kwa ndege maalumu kutoka Dar es Salaam alikokuwa akishikiliwa tangu Jumamosi, baada ya Hakimu Magesa kuamuru akamatwe mara moja kwa yeye na mdhamini wake kutofika mahakamani siku hiyo.
Magesa, alisema, hawezi kumkubali tena mdhamini Maligwe kumdhamini Mbowe, kwani alishindwa kutii amri ya kufika mahakamani, mshitakiwa aliposhindwa kufika.
Baada ya kukubaliwa dhamana na kuachiwa, mamia ya watu waliofurika mahakamani hapo wakiwamo wafuasi wa Chadema, walilipuka kwa shangwe, vifijo na vigelegele na kumbeba hadi nje ya chumba cha mahakama.
Walisikika wakiimba nyimbo zikiwamo zenye ujumbe wa kumkataa Meya wa Manispaa ya Arusha, Gaudence Lyimo.
Akizungumza mahakamani, Hakimu Magesa, alisema kutokana na mdhamini huyo kukiuka masharti ya kuhudhuria mahakamani, kwa sababu kwamba naye anakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Mwanzo ya Maromboso, ameamua kutoa nafasi kwa mdhamini mwingine.
“Mahakama hii imeona kuwa mdhamini huyu ana makosa na hawezi kueleza mahakamani hapa ukweli kuhusu tarehe alizokuwa anahudhuria, tunaona hana sifa za kuwa mdhamini na hivyo tunamkubali John Bayo awe mdhamini wa Mbowe,” alisema Magesa.
Alisema mbali na kusema uongo mahakamani hapo kuwa alikuwa akifika mahakamani, bado Mahakama haina sababu na kuendelea naye kwa sababu tayari ana kesi ya jinai ambayo hatma yake haifahamiki.
Kuhusu Mbowe, Hakimu alisema, ni kweli Mahakama iliruhusu washitakiwa wabunge wahudhurie vikao vya Bunge la Bajeti na hivyo hawana sababu na Mbowe, ila kutokana na kukosekana kwa mdhamini wake, ndiyo sababu walitoa amri ya kukamatwa kwake.
“Ila sasa mtaendelea na vikao vyenu vya Bunge, ila wadhamini wenu lazima waje mahakamani kila kesi itakapotajwa na tunaondoa amri ya kukamatwa na sasa utaendelea na dhamana yako ya awali,” Magesa alimwambia Mbowe.
Kabla ya Hakimu kutoa uamuzi huo, alimpa nafasi Maligwe aeleze sababu za kutofika mahakamani.
Akijieleza, Margwe alidai kuwa Mei 27, hakufika kwa sababu alikuwa na kesi katika Mahakama ya Mwanzo ya Maromboso na Mei 30 alifika mahakamani ila kwa kuwa Mahakama haikumpa nafasi ya kusema lolote, hakujitokeza.
Awali kabla ya uamuzi kutolewa na Hakimu, Wakili wa Utetezi, Method Kimomogoro, aliiomba Mahakama, iondoe amri ya kukamatwa kwa Mbowe na kutaka apewe dhamana yake ya awali, ili aweze kuhudhuria vikao vya Bunge la Bajeti ambalo yeye ni kiongozi wa Upinzani.
Aidha Wakili huyo alimtetea mdhamini wa Mbowe kwa kutofika mahakamani na kudai kuwa hiyo ipo kwa kila mtu na hata wao mawakili husahahu tarehe za mahakama na ndiyo sababu huandika, hivyo kwa mwananchi wa kawaida ni lazima asahau tarehe.
Pia alipinga kauli ya Wakili wa Serikali ya kutaka Mahakama impe onyo Mbowe kwa sababu kosa si lake na Mahakama ilimpa udhuru Aprili 29, kesi hiyo ilipotajwa na kutoa sababu ya kuwa watakuwa katika vikao vya Bunge la Bajeti na kuomba Mahakama imrejeshee dhamana yake ya awali.
Wakili wa Serikali, Juma Ramadhani, aliiomba mahakama hiyo itoe onyo kali kwa mshitakiwa, kwa kutofika mahakamani na pia kumtaka mshitakiwa na wenzake wawe na mawasiliano ya karibu na wadhamini wao, ili wasikose mahakamani hapo.
“Mnajua hii ni kesi ya jinai na kama ni ya jinai lazima muwepo mahakamani na mkikosa lazima wadhamini wawepo, ili kuondoa utata, ila hofu tuliyonayo sisi ni pale tutakaposubiri Mkutano wa Bunge uishe ndipo washitakiwa waje mahakamani … ni muda mrefu sana, hivyo naomba wakili wa utetezi awasiliane na washitakiwa kupata siku ya nafasi ili kutoa maelezo ya awali,” aliomba Ramadhani.
Alisema kwamba kuhusu dhamana ya Mbowe hana shaka nayo, isipokuwa mdhamini wake hana uhakika na hajui nini anachokifanya, hivyo hafai kuwa mdhamini na kuomba Mahakama itoe uamuzi wa mdhamini huyo.
Baada ya pande hizo zote kuzungumza, Hakimu alimwachia huru kwa dhamana Mbowe na kutoa idhini ya kuendelea na Mkutano wa Bunge la Bajeti hadi Juni 24 mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.
Akizungumza na wafuasi wa Chadema pamoja na waandishi wa habari, kwenye viwanja vya Mahakama hiyo, mara baada ya kuachiwa huru kwa dhamana, alisema inasikitisha kuona Serikali inatumia nguvu kubwa ya kumdhibiti kama mhalifu.
Kwa mujibu wa Mbowe, Serikali ilitumia ndege ya Jeshi yenye uwezo wa kubeba watu 100, ambayo ilichukua watu watatu; yeye, Kamishna wa Polisi Kanda ya Ilala na Kamishna wa Polisi wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia wa Tanzania (FFU) hadi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) saa 9 alfajiri kuamkia jana.
Pia alisema mbali na kusafirishwa kwa ndege hiyo kubwa, pia kulikuwa na magari manane ya FFU ambayo yalikuwa na mabomu na silaha kama wanasindikiza mhalifu.
Mbowe alisema hakuwa na kosa la kukamatwa na ndiyo sababu mahakama haikumhoji hata swali moja, kwa sababu waliona mwenye shida ni mdhamini wake.
“Ila mimi naheshimu Mahakama, lakini sitakosa kusema pale wanapokosea, kama vile baadhi ya watumishi wa Mahakama kukubali amri za viongozi wa Serikali, ilimradi tu kutimiza matakwa yao,” alisema Mbowe.
Alisema hakukuwa na sababu za msingi za kutumia rasilimali za Serikali ambazo ni mali za umma kumsindikiza kama mhalifu, mtu ambaye hakuwa na silaha.
“Mimi nasema nawashukuru wananchi na viongozi wote walioshiriki kunitia moyo wakati huu wa siku mbili nilizokaa ndani,” alisema na kuongeza kuwa anaahidi kufanya kazi nzuri katika mkutano wa Bunge la Bajeti unaoanza leo.
Hata hivyo, alisema anawashukuru polisi kutomfanyia unyama, kwani walikaa naye vizuri, isipokuwa alinyimwa haki yake ya msingi ya kuwa na uhuru wa kuwasiliana na watu.
Katika kesi hiyo inayomkabili Mbowe na wabunge 13 wa Chadema, wanadaiwa kuandaa mkutano na kuandamana kinyume cha sheria Januari 2011.
Wengine katika kesi hiyo ni Kabwe Zitto, Halima Mdee, Godbless Lema, Suzan Kiwanga, Ezekia Wenje, Christina Lissu, Paulina Gekulu, Israel Natse, Suzane Lyimo, Joseph Mbilinyi, Rahya Ibrahimu, Joyce Mukya na Joseph Selasini.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na waandishi wa habari jijini hapa, walieleza kusikitishwa na magari na polisi wenye mabomu na silaha, kutanda kona zote za Jiji, kana kwamba kulikuwa na wahalifu wakubwa wanaoletwa jijini. Walidai hali hiyo ilisababisha wasiwasi kiasi cha baadhi ya maduka kufungwa.
Flora Mwakasala anaripoti kutoka Dar es Salaam, kwamba wanachama watatu wa Chadema walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa tuhuma za kuandamana bila kibali na kusababisha uvunjifu wa amani.
Washitakiwa hao ambao walisomewa mashitaka mawili mbele ya Hakimu Sundi Fimbo, ni Jenerali Kaduma, Juliana Daniel na Joseph Msetti.
Kulingana na taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova, Kaduma ni mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na mkazi wa Kijitonyama, Daniel ni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mkazi wa hosteli za Mabibo na Msetti ni mkazi wa Tegeta, Dar es Salaam.
Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda, alidai mahakamani hapo kuwa Juni 5 eneo la Ufipa, Kinondoni, Dar es Salaam, washitakiwa hao na wenzao ambao bado hawajafahamika, walikula njama za kutenda kosa hilo.
Ilidaiwa kuwa juzi saa 11 jioni Magomeni, washitakiwa walifanya mkusanyiko na kuandamana bila kibali, kitendo kilichosababisha uvunjifu wa amani kwa wakazi wa eneo hilo.
Washitakiwa ambao wanatetewa na Wakili Mabere Marando, walikana mashitaka na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hakimu Fimbo alisema dhamana iko wazi endapo washitakiwa watatimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi katika kampuni zinazotambulika, ambao watasaini hati ya Sh milioni nne.
Upande wa mashitaka uliiomba Mahakama iwape muda wa siku moja wapitie na kukagua barua za wadhamini kwa kuwa kipindi hiki kimekuwa na wadhamini waongo.
Hakimu Fimbo aliahirisha kesi hiyo hadi leo, kwa ajili ya kutoa dhamana kwa kuwa wadhamini waliofika walikuwa si waajiriwa na wengine hawakuwa na barua wala vitambulisho vya kazi.
0 Comments