Pichani ni virusi vya HIV.

Mwaka wa 1981, daktari mmoja wa California Marekani aliona vijana wa kiume watano, walioshiriki katika mapenzi ya jinsia moja, wakiwa na ugonjwa usiokuwa wa kawaida.
Walikuwa na homa ya pneumonia na saratani ya ngozi.

Dakta Gottlieb hakujua kuwa ripoti zake, ndio zitakuwa historia ya kwanza kuandikwa juu ya ugonjwa ambao baadae utakuja kuwa janga kubwa la AIDS, au UKIMWI.
Virusi vya HIV viligundulikana miaka miwili baada ya ugunduzi huo wa Dakta Gottlieb.
Tena damu ikaweza kupimwa kama ina virusi vya HIV, na baadae zikapatikana dawa kadha za kudhibiti ugonjwa huo.
Umoja wa Mataifa unakisia kuwa tangu mwaka wa 1981, UKIMWI umeuwa watu milioni 30, na idadi kama hiyo hivi sasa wanaishi na virusi vya HIV.
Lakini juma lilopita, umoja huo uliripoti kuwa idadi ya watu wanaoambukizwa inapungua katika nchi kadha, lakini mamilioni ya wagonjwa bado hawapati dawa wanazohitaji.
Matabibu wanasema virusi vya HIV sasa wanavifahamu sawasawa, na wagonjwa wanaofululiza kula dawa kwa wakati, wanaweza kuishi karibu maisha ya kawaida.