TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars imeondoka alfajiri Juni 3 kwenda Bangui, Afrika ya Kati kwa ajili ya mechi ya kuwania fainali za Kombe la Mataifa Afrika mwakani dhidi ya wenyeji wao CAR.
Msafara wa timu hiyo ukiongozwa na mjumbe wa kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Samuel Nyala, ulitarajiwa kufika mjini Bangui jioni.
Wachezaji walioondoka ni Shaaban Kado, Shaaban Dihile, Shadrack Nsajigwa, Idrisa Rajabu, Amir Maftah, Juma Nyosso, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Aggrey Morris.
Wengine ni Shaaban Nditi, Jabir Azizi, Nourdin Bakari, Nizar Khalfani, Julius Mrope, Mbwana Samatta, John Bocco, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto, Salum Machaku, Mohamed Banka na Athumani Machuppa.
Stars ina kibarua kigumu katika mechi hiyo kwani inahitaji ushindi ili ijiweke sawa katika harakati za kufuzu fainali hizo zitakazofanyika mwakani Gabon na Equatorial Guinea.
Katika mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya CAR iliyofanyika Machi 26 jijini Dar es Salaam, Stars iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Kwa mara ya mwisho Tanzania kushiriki fainali hizo ilikuwa mwaka 1980 zilipofanyika Lagos, Nigeria.
Mpaka sasa kundi B la Stars timu zote zina pointi nne lakini zikitofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa na CAR ndio inayoongoza kundi, ikifuatiwa na Tanzania, Morocco na Algeria.
0 Comments