Tume ya pande tatu kati ya serikali ya Tanzania, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), imefikia kikomo kabla ya shughuli zake, kwa kile kilichoelezwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Shamsi Vuai Nahodha, kuwa ni kushindwa kwa shirika hilo kuheshimu mapendekezo ya kuangalia upya maendeleo ya mchakato wa kuwarudisha wakimbizi.
“Inaonekana watu hawa wako kibiashara zaidi wakati sisi kama serikali tumewekeza rasilimali nyingi kwenye mchakato tukifuata sheria za kimataifa.

Nimeshangazwa kusikia toka kwa uwakilishi wa UNHCR Tanzania kwamba, umepokea maelekezo thabiti toka juu ukiruhusu wakimbizi kuondoka,”
alisema Nahodha jana wakati wa mkutano wa pande hizo kwa ajili ya kupatikana kwa kibali cha kuwarudisha wakimbizi nchini kwao ambapo kibali hicho hakikuweza kusainiwa. Kwa mujibu wa Nahodha, mkutano uliopita ulipitisha Mpango Mkakati wa hatua tatu za kuchukuliwa na wadau ili kuhakikisha wakimbizi wa DRC wanarudi kwa njia iliyo rahisi na yenye utu.
Alisema mkutano uliofanyika Machi mwaka huu, huko DRC walikubaliana kuwahusisha wataalamu ambao hata hivyo wamependekeza kwamba, hali ya usalama DRC imeimarika.
Alisema sheria ya kimataifa inahitaji kutumia njia ya kuwarudisha wakimbizi waliotayari kurudi, kuwasaidia na kuwahamasisha na kwamba njia mbili zimeendelea vizuri mpaka hiyo juzi walipogundua toka kwa UNHCR kwamba kuna maagizo toka juu ya kutoingia katika hatua hiyo ya tatu.
“Sasa kwa kuwa tumekuwa wakarimu vya kutosha na ni kwa misingi ya kibinadamu kuwa serikali inatoa kipindi cha miezi sita ya kuwarudisha kwa mafungu ya watu 10,000 kwa mwezi wakimbizi wa DRC walioko nchini,” alisema.
Kuna wakimbizi wapatao 60,000 katika makambi ya wakimbizi nchini.
Waziri Nahodha alisema DRC itajengwa na Wakongo wenyewe na kwamba Tanzania haiwezi kuendelea kugawana rasilimali kidogo ilizonazo na wakimbizi.”Ni muda mwafaka kwa wakimbizi kuondoka nchini ili wakajiunge na Wakongo wenzao kujenga taifa lao.”
Akiongea na wanahabari baadaye, Mwakilishi wa UNHCR nchini, Oluseyi Bajulaye, alilitoa shirika lake kwenye lawama na akasema kuna mambo ya msingi ambayo hayajafanyiwa kazi na tume hiyo.
Alipobanwa kutoa maoni yake kwamba amepewa maagizo toka kwa wakubwa wake ya kudhohofisha mazungumzo, alisema “Nilichopokea naweza kusema hayakuwa maagizo ila ushauri wa kuuleta mbele ya tume,” alisema.
Bajulaye alipinga kwa nguvu zote kwamba UNHCR iko nchini kibiashara.
Wiki iliyopita, tume ya pande tatu ilikutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi masuala yaliyokuwa yanatatiza na hasa kupata suluhisho la kudumu kwa hali waliyonayo wakimbizi wa Burundi nchini.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI