Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hilary Clinton (kulia) akifurahia jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania , Bernard Membe mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam kwa ziara ya siku tatu nchini. (Picha na Fadhili Akida)
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton aliwasili jana nchini kuanza ziara ya siku tatu. Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere, Kipawa nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam akiwa na msafara wa watu wasiozidi 50, wengi wakiwa wanahabari, Waziri huyo alionekana kupagawishwa na kikundi cha ngoma alichoungana nacho kihisia kwa takribani dakika 13.
Akiwa na mwenyeji wake, Bernard Membe ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Clinton kwa muda wote alionekana akitabasamu na kutikisa kichwa, huku mwili wake pia ukinesanesa.
Waziri Membe ndiye aliyemshitua mama huyo na kuondoka eneo la wacheza ngoma,
tayari kwa safari ya kwenda Hoteli ya Kempinski, katikati ya Jiji.
Mama Clinton, mke wa Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton aliyewasili nchini saa 11:30 jioni na ndege ya Serikali ya Marekani (ubavuni 80002) akitoka Zambia alikohudhuria mkutano wa Mpango wa Soko Nafuu kwa Bidhaa za Afrika (AGOA), leo atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Naibu Waziri Mkuu wa Ireland, Eamon Gilmore.
Katika mazungumzo hayo yatakayofanyika katika Hoteli ya Kempinski, watazungumzia mradi wa ‘Siku 1,000 wa kutokomeza njaa Tanzania’ na kisha baadaye atatembelea shamba la kilimo la Mlandizi, Kibaha, mtambo wa umeme wa gesi wa Symbion uliopo Ubungo na baadaye atakwenda Kituo cha Afya Buguruni .

0 Comments