Waziri Mkuu Mizengo Pinda(pichani) amesema rushwa na umaskini hasa katika bara la Afrika ni matokeo ya uongozi dhaifu wa mifumo ya utawala wa umma isiyo na tija kwenye sekta ya umma na ile ya binafsi.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua kongamano la maadhimisho ya siku ya utumishi wa umma ulimwenguni, barani Afrika na kwa Tanzania ambapo kwa mara ya kwanza sherehe hizo zinafanyika katika ardhi ya Afrika.
Pinda alisema umaskini wa kutupwa katika nchi nyingi kwa sehemu ni matokeo ya uongozi duni kama ilivyobainishwa kwenye ripoti ya maendeleo ya binadamu ya mwaka 2010 ambayo inaonyesha kuwa watu billioni 1.75 katika nchi 104 ni maskini wa kutupwa.
Alisema wengi kati ya watu hao wanaishi Asia ya Kusini (karibu millioni 844) na zaidi ya robo (Millioni 458) wanaishi Afrika.
“Ni ukweli ulio wazi kwamba serikali zenye kujali na zinazowajibika kwa wananchi wake haziteremshi na Mwenyezi Mungu na haziji kwa bahati bali ni zao la viongozi wenye muono na wawajibikaji pamoja na mifumo ya utawala wa umma iliyo ya ufanisi,” alisema
Alisema kwamba tatizo la matumizi mabaya ya madaraka kwa upande wa viongozi au rushwa kama inavyoainishwa na shirika la kimataifa la uwazi (Transparent international) ni kubwa zaidi kwa nchi za Afrika ambapo kwa mujibu wa ripoti hiyo, hakuna nchi katika bara hili ambayo iko kwenye orodha ya nchi 20 zilizofanya vizuri katika kupambana na rushwa ulimwenguni.
Aliwataka viongozi wa serikali za kiafrika na hasa kwenye eneo la utumishi wa umma waweke maslahi ya watu wao mbele ili kuondoa tatizo la umaskini na rushwa.
CHANZO: NIPASHE