BUNGE la Tanzania limeipongeza timu ya soka ya Simba ya Dar es Salaam kwa ushindi wake wa bao 1-0 kwa sifuri dhidi ya timu ya DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mchezo wa Kombe la Shirikisho.
Akisoma ujumbe mfupi wa kumpongeza Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Rage ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema Bunge hilo linajivunia na kufurahishwa na ushindi huo wa Simba.
“Kwa kweti tunaipongeza timu ya Simba kwa ushindi wake, namuona mheshimiwa Rage ameonesha uzalendo kwa kuvaa nguo nyekundu, naitakia ushindi na baraka zote
katika michezo yake mingine,” amesema Makinda huku akishangiliwa.
Rage wakati wote alikuwa akitabasamu akiwa amevaa koti lake jekundu ndani ya ukumbi huo.
Simba Jumapili iliifunga DC Motema Pembe katika mchezo wa Kombe la Shirikisho uliofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kujiweka katika matumaini ya kufuzu hatua ya makundi.
Timu hizo zitarudiana Jumamosi wiki hii mjini Kinshasa, DRC, ambapo ili isonge mbele Simba itahitaji sare ya aina yoyote.
Mshindi wa mchezo wa Simba na Motema Pembe atakuwa Kundi B la michuano ya Kombe la Shirikisho pamoja na timu za JS Kabylie ya Algeria, Moghreb Fes ya Morocco na Sunshine Stars ya Nigeria.

0 Comments