AJALI za barabarani zimeendelea kukatisha uhai wa maisha ya Watanzania baada ya watu
watano kufariki dunia juzi na wengine 18 kujeruhiwa kutokana na basi ya Kampuni ya Kazuge Coach kupata ajali wilayani Nzega mkoani Tabora.

Basi hilo lenye namba za usajili T933 AHK, aina ya Scania linalofanya safari zake kati ya Urambo na Igunga mkoani hapa, lilipata ajali katika Kata ya Mogwa, Tarafa ya Bukene wilayani Nzega saa 12 jioni.


Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Liberatus Barlow, waliokufa ni wanaume wawili, wanawake watatu akiwemo na mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja.


Aliwataja waliokufa ni Adam Abdulrahman (28) na Hussein Selemani (31) wote wafanyakazi wa basi la Zuberi waliokuwa wakiishi Tabora.


Alisema jitihada za kuyapata majina ya marehemu wengine zinaendelea.


Kamanda Barlow alisema, chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa basi hilo ambalo

dereva wake jina lake halikuweza kutambulika mara moja, alitoweka katika eneo
hilo la tukio baada ya ajali hiyo.



Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Dk. Timoth Ng`wandu alisema majeruhi katika ajali hiyo ni 18 ambapo majeruhi amesafirishwa kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.


Alimtaja majeruhi huyo kuwa ni Zainabu Rashidi (20), mkazi wa Rusinge wilayani Urambo ambaye amevunjika miguu yote, mkono mmoja na kuteguka kiuno, hivyo kuhitaji matibabu ya hali ya juu.


Dk. Ng’wandu alisema majeruhi wengine wanaendelea vizuri na matibabu.


Kamanda Barlow aliwataka madereva kufuata taratibu za barabara katika safari ndefu na fupi ili kuepusha ajali zisizo za lazima kama ajali hiyo ambayo alisema sehemu ilipopata ajali ni nzuri isiyo na matatizo, lakini kwa uzembe wa dereva alishindwa kumudu basi hilo hatimaye

kuhatarisha maisha ya watu na wengine kupoteza maisha papo hapo.

Mkoani Mbeya, Mwandishi Wetu, Neema Kidumba anaripoti kuwa mwanafunzi wa Darasa la Tatu katika Shule ya Msingi Ihanda wilayani Mbozi, Philipo Tuya (13) amepoteza maisha papo hapo baada ya kugongwa na gari akivuka barabara.


Mwanafunzi huyo alipatwa na mauti hayo juzi saa 12 jioni katika maeneo ya Ihanda katika Barabara Kuu ya Tunduma - Mbeya.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi alisema ajali hiyo ilihusisha gari lenye namba za usajili T266 BNC, lililokuwa likiendeshwa na Salimu Mahoho (38) mkazi wa jijini Dar es Salaam.


Anadaiwa alikuwa akiendeshwa kwa mwendo kasi na anashikiliwa na Polisi pamoja
na gari lake.