HOTUBA YA MHE. ROSTAM AZIZ KWA WAZEE WA IGUNGA - TABORA
UTANGULIZI
WAZEE wangu, kwanza kabisa kabla ya kueleza kile ambacho kimenisukuma kuzungumza nanyi leo, napenda kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kufikia siku hii ambayo inatukutanisha waja wake.

Wazee wangu wa Igunga, baada ya kufanya hivyo napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru ninyi nyote mmoja mmoja na katika umoja wenu kwa kuitikia wito wangu, kijana wenu, niliyewaomba nije nizungumze nanyi siku hii ya leo.

Nafanya hivyo nikitambua vyema kwamba, kama si nyinyi wazee wangu na wengine wengi ambao hatuko nao hapa leo kwa sababu mbalimbali, ambao mmekuwa na imani kubwa nami nisingeweza kufikia hapa nilipofika sasa.

Wazee wangu, waasisi wa taifa letu walitufundisha kutambua na kuheshimu ukweli kwamba; ‘Uongozi ni Dhamana’ dhana ambayo kila ninapokaa na kutafakari huwa inanirejesha nyuma na kukumbuka jinsi nyinyi mlivyokaa katika umoja wenu na kuniteua mimi, miongoni mwa vijana wenu wengi, kuwa mwakilishi wa Jimbo la Igunga tangu mwaka 1994.

Katika kipindi hicho chote cha utumishi wangu, nyinyi wazee wangu mmekuwa mhimili muhimu ambao umeniwezesha kutimiza wajibu wangu kwa bidii kubwa, maarifa na nidhamu ya hali ya juu nikitambua namna ambavyo mmekuwa na imani kubwa juu yangu.

Ari na moyo wa imani, ushirikiano na mshikamano ambao wazee wangu mmekuwa nao kwangu ndiyo ambao kwa kiwango kikubwa umetuwezesha kufanya kazi kwa pamoja, tukishinda changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikilikabili jimbo letu katika kipindi chote ambacho mmeendelea kuniamini kuwa mbunge wenu kwa miaka 18 sasa.

Wakati nikitambua na kuheshimu ukweli kwamba katika kipindi chote cha ubunge wangu mmekuwa na imani kubwa nami na kuniunga mkono kwa dhati, naamini kwamba kwa upande wangu pia nimejitahidi kwa kadiri nilivyoweza, kutimiza matarajio ya wananchi wa Igunga.

Miongoni mwa mafanikio makubwa tuliyoyafikia kupitia ushirikiano wetu na uongozi wa pamoja ni kwamba, mwaka 1994 Igunga ilikuwa ni wilaya ya mwisho kwa maendeleo mkoani Tabora lakini leo ndiyo ya kwanza, taa za barabarani, bima ya afya kwa kila kaya, zahanati kila kijiji na shule nyingi kuliko idadi ya kata zilizomo kwenye wilaya.

Wazee wangu, nayasema haya nikitambua kwamba, kama ilivyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, mafanikio makubwa tuliyoyapata katika nyanja za elimu, afya, makaazi bora na kilimo katika kipindi chote ambacho mmendelea kuniamini kuwa mbunge wenu kwa miaka 18 sasa.

Wakati nikitambua na kuheshimu ukweli kwamba katika kipindi chote cha ubunge wangu mmekuwa na imani kubwa nami na kuniunga mkono kwa dhati, naamini kwamba kwa upande wangu pia nimejitahidi kwa kadiri nilivyoweza, kutimiza matarajio ya wananchi wa Igunga.

Wazee wangu, nayasema haya nikitambua kwamba, kama ilivyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, mafanikio makubwa tuliyoyapata katika nyanja za elimu, afya, makaazi bora na kilimo katika kipindi hicho chote hayajaweza kumaliza changamoto zote za maendeleo ambazo zinatukabili.

Wazee wangu, ingawa nimekuwa na kawaida ya kukutana na kuzungumza nanyi mara kwa mara, mmoja mmoja na wakati mwingine katika umoja wenu, wito wangu wa leo una makusudi ambayo kwa kiwango kikubwa ni tofauti na yale ambayo tumeyazoea.

Japokuwa ujumbe ninaotaka kuzungumza nanyi wazee wangu, si mgeni sana masikioni mwenu, tofauti ya leo na mikutano yetu mingine iliyopita ni uamuzi ambao nimekusudia kuufanya na ambao nitayatangaza muda mfupi ujao.

YATOKANAYO

Wazee wangu, naamini mmekuwa mkifuatilia kwa karibu hali ya siasa nchini na hususani afya ya kisiasa na matukio mengine ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho mimi ni mwanachama wake na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) nikiuwakilisha Mkoa wetu wa Tabora.

Naamini kwamba katika kufuatilia kwenu mtakuwa mmebaini kuwapo kwa matukio ambayo kwa namna moja au nyingine yamekuwa yakitokea huku yakiligusa jina langu na wakati fulani nafasi yangu kama kiongozi wa chama hicho.

Wazee wangu, nayasema hayo kwa sababu mara kwa mara ninapokutana nanyi nikiwa katika ziara zangu jimboni na wakati mwingine mnapowasiliana nami kwa njia mbalimbali mmekuwa mkionesha kuguswa kushitushwa na kutaka kujua kulikoni kuhusu mambo hayo yanayotokea.

Mimi, kama mnavyonijua nyote, ni mtu muwazi na mkweli. Siku zote nimekuwa mwepesi sana wa kuwaeleza kuhusu kila kinachotokea ili kuwaondoa hofu na wakati huo huo kuwahakikishia kwamba masuala yasiyo na msingi hususani yale yanayogusa siasa za kitaifa hayawezi kutuondoa katika mstari sahihi wa kuwahudumia wananchi wa Igunga, mkiwamo nyinyi wazee wangu ambao mmeniamini na kunituma kuwawakilisha.

Nyinyi wenyewe ni mashahidi wazuri kwamba tangu matukio yanayogusa jina langu yaanze kutokea miezi michache tu baada ya Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikweti kuingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005, tumekuwa tukiyapuuza na tukaendelea kufanya kazi pamoja kwa bidii.

Bado naamini na nitaendelea kuamini kwamba tulifanya uamuzi sahihi wa kuyapuuza matukio hayo kwani mbali ya kuendelea kutimiza malengo mbalimbali yaliyokuwamo katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM, pia mliendelea kuniamini kwa nafasi yangu ya kuwa mwakilishi wenu bungeni na hata mkaniruhusu nibebe jukumu jingine kubwa la kuwa Mjumbe wa NEC ninayewakilisha mkoa wetu wa kihistoria wa Tabora.

Wazee wangu, nyinyi ndiyo watu mnaolifahamu vyema jimbo letu la Igunga na hakika nyinyi ni sehemu muhimu ya watu wanaojua historia ya kisiasa ya Mkoa wa Tabora kwa miaka mingi hata kabla ya kuja kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini.

Hakuna shaka hata kidogo kwamba, Tabora ni kitovu hasa cha uasisi wa siasa za vyama vingi hapa nchini. Ni wazi kwamba huwezi ukazungumzia chimbuko la vyama vya upinzani tunavyoviona hapa nchini leo pasipo kugusa mkoa huu ambao umekuwa chimbuko la wanasiasa wenye mizizi hapa na nchini kwa ujumla.

Majina ya wanasiasa wa aina ya wazee wetu, hayati Chifu Said Abdallah Fundikira na Christopher Kassanga Tumbo, Kasela Bantu (Mungu awalaze mahala pema peponi), James Mapalala, Profesa Ibrahim Lipumba na mengi mengine yana mizizi yao katika Mkoa wetu wa Tabora.

Kutokana na ukweli huo basi ni wazi kwamba, nikiwa Mbunge wa Igunga kwa vipindi vinne mfululizo na wakati huo huo nikiwa Mjumbe wa NEC kwa vipindi vitatu mfululizo, moja ya kazi ambazo nimezifanya kwa uaminifu na kwa bidii kubwa huku nikiungwa mkono na kushirikiana nanyi ni ile ya kuhakikisha kwamba mkoa huu pamoja na kuwa kitovu cha upinzani unaendelea kubakia kuwa ngome muhimu ya kisiasa ya CCM.

Si vibaya tukakumbushana kwamba, wakati nachaguliwa kuwa mjumbe wa NEC wa Mkoa mwaka 1997, jimbo moja katika mkoa wetu lilikuwa likishikiliwa na upinzani. Leo hii Tabora ni mkoa pekee miongoni mwa mikoa iliyotuzunguka ambao haukupoteza jimbo hata moja kwenda upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa 2010. Mafanikio haya tuliyafikia kwa pamoja kutokana na ushirikiano wenu wazee wangu.

Wazee wangu, Waswahili wanasema usione vyaelea, vimeundwa. Kazi ya kuijenga CCM katika mazingira yenye mizizi hasa ya upinzani nikiwa mbunge na hususani M-NEC kutoka Mkoa wa Tabora haijapata kuwa rahisi na itaendelea kuwa ngumu na ambayo mapambano yake ni makali sana.

Wazee wangu, kwa namna ya pekee kabisa napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru nyinyi wazee wangu wa Igunga na wananchi wenzangu wote wa Mkoa wa Tabora kwa kushikamana na kuifanya kazi hiyo kwa bidii, uaminifu na mafanikio makubwa.

Matunda ya kazi hiyo kubwa yanaonekana. Pamoja na kuwa kitovu cha kihistoria cha siasa za upinzani, Tabora ndiyo mkoa pekee katika eneo hili ambao unaongozwa na wabunge wote kutoka CCM baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na hata kabla ya hapo.

Kwa sababu hiyo basi, wazee wangu, sote katika umoja wetu ukiacha mafanikio makubwa tuliyopata katika jimbo na Wilaya yetu ya Igunga, tunayo mambo mengine ya msingi ya kujivunia. Kwa moyo wa dhati na kwa unyenyekevu mkubwa napenda kuwapongeza kwa namna mlivyojitoa kukipigania na kukitetea chama chetu kwa ari na nguvu ya kipekee.

KUJIVUA GAMBA

Wazee wangu, chama chetu chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kimeamua kwa kauli na nia moja kujitathmini na kufanya mabadiliko makubwa ya kimfumo yenye lengo la kukiwezesha kiendelee kubakia chama kinachoaminiwa na kuungwa mkono na Watanzania walio wengi.

Dhamira ya mwelekeo huo wa kufanya mabadiliko ya ndani ya chama chetu ilitangazwa rasmi na Mwenyekiti wetu Rais Kikwete wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, mjini Dodoma.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete aliyafananisha mabadiliko hayo na tabia ya kawaida na ya asili ya nyoka na wanyama wengine kadhaa ya ‘Kujivua Gamba’.

Wazee wangu hatua ya kwanza ya utekelezaji wa azimio hilo na mwelekeo huo sahihi ilifanyika mjini Dodoma wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya Taifa ya CCM ambacho mimi nilikuwa mjumbe wake.

Wakati wa kikao hicho, wajumbe wote wa Kamati Kuu na wale wa Sekretarieti ya chama chetu wa wakati huo kwa kauli moja tulikubaliana kujiuzulu, lengo likiwa ni kumpa Mwenyekiti wetu fursa nzuri ya kufanya mabadiliko ya uongozi yatakayotoa nafasi ya kupata mwelekeo mpya wa Chama.

Wazee wangu, tulifanya hivyo tukionesha kuunga mkono kwa asilimia 100 kile ambacho bado naendelea kuamini kuwa ni mawazo sahihi na yenye mwelekeo thabiti ya Mwenyekiti wetu ambayo kwa kiwango kikubwa yalikuwa yakiakisi matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa urais, ubunge na udiwani wa Oktoba mwaka jana.

Niliseme kwa maneno machache tu hili. Ingawa ni kweli kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana umekirudisha madarakani chama chetu kwa kukipa ushindi mkubwa katika uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani kwa Tanzania Bara na Zanzibar, kiwango cha ushindi tulichopata kimeonyesha waziwazi dalili za wananchi kupunguza imani yao kwetu kuilinganisha na ilivyokuwa mwaka 2005.

Tungekuwa ni chama cha siasa cha ovyo iwapo tungepuuza kupungua kwa kura za rais kutoka zaidi ya asilimia 80 tulizopata mwaka 2005 hadi kufikia aislimia 61 mwaka jana kiwango ambacho ni pungufu kwa asilimia 20 ya kura katika kipindi cha miaka mitano tu, hasa ikizingatia ukweli kwamba mgombea urais ni mtu yule yule.

Tungekuwa ni chama cha siasa kilichokosa umakini iwapo tungekaa pasipo kuchukua hatua zozote za kujiimarisha baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu kuonesha wazi kukua kwa upinzani ambao umeongeza idadi ya wabunge na madiwani katika pande zote mbili za muungano.

Matokeo hayo ya uchaguzi ambayo hapana shaka yamekitikisa chama chetu yalitukumbusha wasia ambao tuliachiwa na Baba wa Taifa aliyesema; ‘Bila ya CCM Madhubuti Nchi Yetu Itayumba’.

Wazee wangu, kwa sababu ya kutambua ukweli kwamba hakuna haki isiyo na wajibu kama nilivyosema awali, mimi na wenzangu tuliokuwa katika Kamati Kuu tuliona ulazima, haja na umuhimu wa kukubali kwa kauli moja wito wa kututaka tujiuzulu ikiwa ni hatua moja ya kujipanga na kukijenga upya chama chetu.

KUJIVUA GAMBA KWAPOTOSHWA

Wazee wangu, kilichotokea baada ya kujiuzulu kwetu kila aliye ndani na nje ya chama chetu amekisikia na anakifahamu. Chama kilipata safu mpya ya uongozi iliyotokana na kuundwa kwa Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu wetu mpya, Mhe. Wilson Mukama, na Kamati Kuu iliyokuwa na sura tofauti na ile ya awali.

Wakati tukitafakari na kuangalia mustakabali mpya wa kisiasa ndani ya chama chetu, ghafla yalianza kutokea mambo ambayo chokochoko zake zilianza kusikika tangu tukiwa ndani ya Kamati Kuu ambayo ilijiuzulu baadaye.

Mara tu baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho kilichagua wajumbe wapya wa Kamati Kuu na kuidhinisha uundwaji wa Sekretarieti mpya, dhana ya kujivua gamba ambayo naamini Mwenyekiti wetu aliianzisha kwa nia njema ilianza kuenezwa ikichukua tafsiri na mwelekeo tofauti na ule wa awali.

Wajumbe wawili wa Sekretarieti, Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Mhe. John Chiligati, na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Mhe. Nape Nnauye, walisikika wakitangaza kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuwa imefikia uamuzi wa kuwapa siku tisini wale walioitwa watuhumiwa wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi ndani ya chama kujitoa katika nafasi zao za uongozi vinginevyo watafukuzwa na chama.

Wazee wangu, baada ya kushinikizwa sana na vyombo vya habari wawataje kwa majina wanasiasa waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi ambao ni wajumbe wa NEC na ambao wanapaswa kujiuzulu nyadhifa zao, wajumbe hao wa Sekretarieti walikwenda mbele zaidi.

Baada ya awali kuwaeleza waandishi wa habari kwamba majina ya watuhumiwa hao yalikuwa yakifahamika kutokana na kuhusishwa katika kashfa tofauti kama zile za Richmond, EPA na ununuzi wa rada, mwishoni viongozi hao walikaririwa wakiyataja majina ya wanasiasa watatu kuwa ndiyo ambao walikuwa wakilengwa na maamuzi hayo.

Wazee wangu, nilishangazwa na kushitushwa na namna porojo na fitina za kisiasa zilivyofinyangwa kwa mara nyingine tena baada ya kusikia jina la mbunge wenu ambaye ni mimi, likitajwa kuwa miongoni mwa yale matatu ya viongozi waliokuwa wakitakiwa eti kupima wenyewe na kisha kuchukua uamuzi wa kujiuzulu nafasi zao za uongozi ndani ya NEC katika kipindi cha siku tisini.

Niliseme hili mapema. Mshangao na mshituko wangu haukusababishwa na kutajwa kwa jina langu, la hasha, bali namna uamuzi halisi wa NEC na hususani dhana nzima ya ‘kujivua gamba’ ilivyoweza kupindishwa na wajanja wachache na kisha kuendeshwa kwa maslahi binafsi ya kikundi fulani cha watu.

Pili, nilishangazwa na kushitushwa na hatua ya viongozi wa chama changu ambacho nimekitumikia kwa bidii na uaminifu mkubwa kufanya juhudi kubwa hata kukivisha kikao kitukufu cha NEC uamuzi ambao msingi wa hoja zake ni vita vya kimakundi ya kisiasa yaliyo ndani ya CCM kwa upande mmoja na propaganda za vyama vya siasa vya upinzani na vyombo vya habari kwa upande mwingine.

Tatu, nilishangazwa na kushitushwa na ujasiri ambao umekuwa ukioneshwa na baadhi ya viongozi wetu wapya wa Sekretarieti wanaolitaja jina langu na kulihusisha na kile wanachokiita ufisadi ambao hata ukweli wa kimazingira na kihistoria ukiachilia mbali ushahidi wa wazi umeshathibitisha kwamba ni porojo za kisiasa zilizotokana na makovu na matarajio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule ujao wa 2015.

Wazee wangu, nyinyi ni mashahidi kwamba, mbali ya mimi mwenyewe kujitokeza kupitia vyombo vya habari na kueleza wazi kwamba sijapata kujihusisha katika vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa maadili ya uongozi au vya rushwa, hakuna ushahidi wowote uliotolewa unaonihusisha na kashfa yoyote miongoni mwa zile zilizotajwa.

Wazee wangu, ni wazi kwamba kama chama chenye siasa chenye dhamana ya kuwaoongoza Watanzania kutoka katika lindi la ufukara, maradhi, matatizo ya makaazi na mengineyo siku zote tunapaswa kuwa makini katika kuhakikisha kwamba changamoto za kuwaongoza na kuwakomboa wananchi waliotupa dhamana hazitikiswi na mawimbi ya matakwa ya nyakati ama ya vyombo vya habari au wapinzani wetu wa kisiasa walio nje ya CCM.

Ni kwa sababu ya kulitambua hilo na hasa kuyatambua madhara yanayoweza kukipata chama chetu na nchi yetu iwapo tutaendekeza siasa za kupakana matope pasipo na sababu za msingi, kuchafuana kusikokoma na kulipizana kisasi ndiyo maana nimeona nitumie fursa hii kuzungumza nanyi wazee wangu ili kuweka kumbukumbu sahihi.

MAAMUZI YANGU

Wazee wangu, nimetafakari sana na kimsingi nimefikia hatua ya kupima yale ambayo yamekuwa yakisemwa na kuandikwa juu yangu na ambayo kwa mtazamo wangu unaoungwa mkono na wanafamilia yangu, marafiki zangu na washirika wangu wa kibiashara walio ndani na nje ya nchi, naona umefika wakati muafaka wa kuchukua hatua.

Kwa sababu ya kutambua uzito wa hatua ninazokusudia kuzichukua, niliona halitakuwa jambo la hekima hata kidogo iwapo ningefanya hivyo pahala pengine popote bali hapa Igunga mbele ya nyie wazee wangu.

Baada ya kukaa na wanafamilia yangu, marafiki na washirika wangu wa kibiashara niliona halitakuwa jambo la busara hata kidogo kuendelea kuvutana na viongozi wa chama changu na wanachama wenzangu wa CCM katika mambo ambayo yanaweza kumalizwa kwa njia muafaka.

Wazee wangu, sina budi niwaeleze kwamba, mbali ya athari za kisiasa na kifamilia, vita vya ovyo vya kisiasa kama hivi tunavyoviendesha na kuviendeleza ndani ya CCM na ndani ya nchi yetu huwa vina athari kubwa katika ulimwengu wa kibiashara. Athari kama hizo za kibiashara huingia ndani zaidi kuliko vichwa vya habari vya magazeti vinavyolenga kuchafuana, na athari hizo huwa kubwa zaidi kwa mtu kama mimi kwa sababu tofauti na wengine wengi hapa nchini, mimi ni mfanyabiashara wa kimataifa.

Katika ulimwengu wa kibiashara wa leo, vita hivi ambavyo vinaweza kuonekana kuwa ni vidogo tu vyenye malengo ya kuchafuana kisiasa, vinakuwa na athari kubwa katika uhusiano wa kibiashara kuliko hata wale wasioelewa wanavyoweza kukadiria. Ndiyo maana nimeona ni afadhali sasa niwape nafasi wale wanaoendesha siasa hizi uchwara na zisizo na tija waendelee na siasa zao hizo ambazo kwa bahati mbaya kwao, mimi sina muda nazo na siwezi kuwa sehemu yake. Na mimi kwa upande wangu niendelee na maisha yangu.

Kutokana na ukweli huo na sababu zote hizo basi, kwa moyo wa dhati na kwa nia thabiti, hatua ya kwanza niliyoiona kuwa ninapaswa kuichukua ilikuwa ni hii ya kuitikia wito unaotokana na msukumo wa ndani ya nafsi yangu wa kuamua kukomesha kabisa malumbano na mivutano isiyo na manufaa kwangu binafsi, kwa viongozi wa chama changu na chama chenyewe.

Msukumo huo si mwingine bali ni ule wa kuamua kuachia nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama, nikianzia na ile ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nikiuwakilisha Mkoa wa Tabora na hii ya ubunge wa Igunga ambazo kama si kwa baraka za chama changu nisingelikuwa nazo.

Napenda kuliweka hili sawa sawa. Uamuzi wangu wa kuachia nafasi zangu zote za uongozi nilizopata kwa tiketi ya CCM haukutokana na wala haumaanishi kukubaliana na shinikizo lililopotoshwa kuhusu azma ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, la hasha, bali dhamira ya dhati ya kuachana na siasa hizi uchwara (gutter politics) na kutumia muda wangu kushughulika na biashara zangu.

Aidha, nimefikia uamuzi huo lengo likiwa ni kuwajengea heshima na imani machoni mwa wanachama na wananchi wengine, viongozi wangu ambao naamini baada ya mimi kujitoa watapata fursa ya kutafakari upya changamoto nyingine mbadala zinazowakabili ambazo msingi wake ni dhamana kubwa walizo nazo za kukiongoza chama chetu na nchi yetu kupitia Serikali yake.

Wakati nachukua uamuzi huu, natambua vyema kwamba, watatokea watu ndani ya chama chetu na nje ambao watafanya kila juhudi kupotosha au kupindisha ukweli kuhusu hatima yangu ya kisiasa baada ya kujiweka kando na kujipa mimi mwenyewe na chama changu fursa ya kutafakari kwa kina majaaliwa yangu na ya nchi yangu katika siku zijazo.

Nafanya hivyo nikiwa na imani thabiti kwamba, uamuzi wangu huu, hususani ule wa kuachia nafasi yangu ya ubunge, yatakipa fursa nyingine CCM ya kuendelea kuliongoza jimbo letu la Igunga katika kipindi cha miaka minne ijayo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kwa upande mwingine, uamuzi wangu huu naona ni fursa kwa viongozi wa Chama changu cha CCM kutafakari na kuamua njia wanayoiona wao ni sahihi kuichukua kwa hatima na mustakabali wa chama chetu na ambayo wanaamini itakipa nguvu mpya ya kisiasa dhidi ya vyama vya upinzani.

Sambamba na hilo, ninayo imani thabiti kwamba, uamuzi wangu wa kubakia kuwa mwanachama wa kawaida na mtiifu wa CCM utakuwa chachu kwa chama changu na kwa Serikali yake kuwatumikia wananchi kwa Ari Zaidi, Kasi Zaidi na Nguvu Zaidi.

Mwisho kabisa, nikimalizia naomba nitumie fursa hii kutoa heshima za pekee kwa Rais Jakaya Kikwete kwa kazi kubwa aliyoifanyia na anayoendelea kuifanyia nchi yetu. Amefanya mengi na makubwa kuiendeleza nchi yetu na watu wake kuliko inavyothaminiwa na kufahamika. Kazi yake kubwa inashindwa kuthaminiwa na kufahamika kutokana na siasa chafu tunazoziendesha Tanzania. Wasia wangu kwa wanasiasa wenzangu, waandishi wa habari na Watanzania wenzangu kwa ujumla ni kuwa tunahitaji kuisaidia nchi yetu kwa kufanya siasa zenye mwelekeo wa kujenga ambazo ndiyo hasa zinapaswa kuwa siasa kwa maana halisi ya neno hilo.

Wazee wangu, baada ya maelezo hayo, nawashukuru sana kwa kunisikiliza na kunielewa.

Ahsanteni sana.