Marekani imesitisha msaada wa dola milioni $350m (£213m) kwa Malawi baada ya maafisa wa usalama kushtumiwa kwa mauaji ya waandamanaji dhidi ya serikali wiki iliopita.
Shirika la Marekani, Millennium Challenge Corporation (MCC), limesema kuwa pesa hizo zilikuwa zitumike katika kustawisha sekta ya nishati ya Malawi.
Lakini wakasitisha msaada huo kwa sababu "walikerwa sana" na mauaji ya watu 19 wakati wa maandamano.
Maandamano hayo ya nchi nzima yalikuwa ni ya kupinga kupanda kwa bei za bidhaa nchini Malawi.
Rais Bingu wa Mutharika alishtumu waandamanaji kwa uhaini na kuamuru wanajeshi pamoja na polisi wa kupambana na fujo kupelekwa katika miji mitatu - mji mkuu, Lilongwe, mji mkubwa zaidi, Blantyre, na Mzuzu ulioko kaskazini.
Makundi ya kiraia yanashtumu maafisa wa usalama kwa kushambulia waandamanaji kwa risasi.

Wanasema hata watu waliokuwa wamesimama walikuwa miongoni mwa waliouawa.
'Uporaji'

Maafisa walisema watu takriban 500 walikamatwa kufwatia maandamano hayo.
Zaidi ya watu 250 walifikishwa katika mahakama mbali mbali nchini siku ya Jumanne kwa mashtaka ya kuchoma moto, uporaji na uwizi, mwandishi wa BBC mjini Blantyre, Raphael Tenthani alisema.
Msemaji wa polisi John Namalenga alisema wale waliofikishwa mahakamani mjini Lilongwe walinyimwa dhamana.