BUNGE limeipongeza timu ya Yanga kwa kutwaa Kombe la Kagame na kuweka heshima ya nchi.
Pongezi hizo zilitolewa bungeni jana na Spika wa Bunge, Anne Makinda muda mfupi baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.
Makinda pia aliipongeza Simba kwa kushiriki fainali hizo na kufanya kombe hilo kubakia nchini hata kabla ya mshindi, Yanga kupatikana.
Kabla ya kutoa pongezi hizo, mmoja wa wabunge mshabiki wa Simba ambaye hakutajwa jina, alipeleka tangazo lililosomwa na Spika la kuipongeza Simba kwa kuwa bingwa wa kombe hilo mara sita.
Baada ya hapo, mbunge mwingine mshabiki wa Yanga ambaye pia hakutajwa jina, alitoa tangazo la kuwaandalia wabunge mashabiki wa Simba sherehe za kuipongeza Yanga kwa ushindi wake wa bao 1-0 bila dhidi ya Simba.
Katika tangazo hilo, mbunge huyo aliwataja baadhi ya wabunge waalikwa katika sherehe hiyo kuwa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Mbunge wa Tabora, Ismail Rage (CCM), ambaye pia ni Mwenyekiti wa klabu ya Simba na Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (CCM).
Wengine walioalikwa ni Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azzan (CCM), Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu Azzan (CCM), Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) na Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF). Yanga juzi iliifunga Simba katika mchezo wa fainali ya Kombe la Kagame uliofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, hivyo kuibuka bingwa wa kombe hilo.
0 Comments