Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete(Pichani juu), anatarajia kuwasha mshumaa usiku wa keshokutwa katika ofisi ndogo makao makuu ya chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam ikiwa ni ishara ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara yatakayoadhimishwa na chama hicho Julai 7.
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema jana kuwa sherehe hizo zitaadhimishwa na chama hicho nchi nzima lengo likiwa ni kukumbuka kazi ya kutafuta uhuru iliyofanywa na Chama Cha Tanganyika African National Union (Tanu).

Alisema katika maadhimisho hayo Rais Kikwete anatarajia kukutana na mabalozi wa nyumba kumi kumi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema sherehe hizo pia zitaandamana na shughuli mbalimbali zitakazofanywa na chama hicho ikiwa ni njia mojawapo ya kuienzi Tanu, ambapo kauli mbiu yake ni Uhuru na Kazi.
Alisema shughuli zitakazofanywa siku hiyo ni pamoja na kufanya usafi, kupanda miti, kusaidia ujenzi na kutembelea wagonjwa.
Aidha, alisema usiku wa kuamkia Julai 7, vijana wa CCM nchi nzima watakutana maeneo mbalimbali kufanya shughuli kadhaa za maadhimisho ya kuzaliwa Tanu.
Alisema mbali na shamrashamra pia kutakuwepo na matamasha yatakayowashirikisha vijana, wasomi, wanasiasa na hata wazee ili kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujikumbusha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru.