Taarifa zasema watu saba wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kwenye mlipuko uliotokea OSLO nchini Norway.
Inaaminiwa kuwa kuna Uhusiano wa moja kwa moja kati ya shambulio hilo na tukio la mtu aliyefyatua risasi katika kambi ya vijana inayoondeshwa na chama tawala cha Leba huko kaskazini magharibi mwa Norway ambapo watu wasiopungua wanne wamejeruhiwa.
Mlipuko huo mkubwa umebomoa majengo ya serikali katika mji mkuu wa Norway, Oslo.
Waziri Mkuu Jens Stoltenberg, ambaye ofisi zake zimeharibiwa vibaya, alieleza hali hiyo kama “nyeti mno”, na polisi imemshauri Waziri Mkuu asiseme yuko wapi.
Maafisa wamesema baadhi ya watu bado wako ndani ya majengo yaliobomoka, baadhi yake yakiwa yanawaka moto.Hakuna aliyedai kuhusika na shambulio hilo.
Picha za televisheni kutoka eneo hilo zilionyesha vifusi na vigae vya madirisha mabarabarani – moshi ukifuka kutokea baadhi ya majengo ambamo mioto ikiwaka. Mabaki ya gari moja lililolipuliwa yalikuwa barabarani.
Barabara zote kuingilia katikati ya mji zimefungwa, liliseme shirike la utangazaji la taifa, NRK, na maafisa wa usalama waliwahamisha watu kutoka eneo hilo, kwa kuhofia mlipuko mwingine.
Msemaji wa hospitali ya Chuo kikuu cha Oslo, amesema watu saba wamepelekwa huko kwa matibabu.Kwa mujibu wa msemaji wa serikali, Hans Kristian Amundsen, Ijumaa hii ni siku ya mapumziko katika Norway hivyo ofisi hazikuwa na shughuli sana kama ilivyo kawaida. Lakini kila siku mamia ya watu huwa ndani ya majengo hayo.
Na mkuu wa mawasiliano wa tawi la chama cha msalaba mwekundu Norway, Oistein Mjarum, amesema ofisi zao ziko karibu na mahali pa mlipuko. Mlipuko huo mkubwa uliweza kusikika katika mji mkuu wote Oslo, aliiambia BBC. Bw Mjarum amesema watu wote mjini Oslo na Norway wameshtuka.
0 Comments