Kristalina Georgieva.

Mjumbe wa Umoja wa Ulaya anayeshughulika na misaada ameanza safari nchini Kenya na Somalia, akisema kuwa ukame uliokumba eneo hilo ni janga kubwa.
Huku njaa imeshatangazwa na Umoja wa Mataifa katika maeneo mawili ya Somalia, mjumbe huyo, Kristalina Georgieva, alisema hali sasa ni mbaya na ni sawa au imezidi ile iliyotokea wakati wa njaa katika Pembe ya Afrika, miaka 19 iliyopita.

Bi Georgieva aliiambia BBC kwamba wapiganaji wa Kiislamu wa Al- Shabaab, wanaodhibiti sehemu kubwa ya Somalia, wataendelea kutatiza juhudi za kufikisha msaada kwa wale wanaouhitaji nchini humo:
"Al-Shabaab wamesharuhusu baadhi ya msaada katika maeneo wanayodhibiti.
Al-Shabaab siyo wote ni wamoja.
Lakini ni tatizo, na wataendelea kuwa tatizo kwa sababu wamesema wazi tangu mwaka wa 2008, kwamba hawataki watu kutoka mataifa ya magharibi, hawataki wasaidizi katika maeneo wanayodhibiti."