Simba waliifunga timu iliyokuwa imeshaaga mashindano ya Etincelles ya Rwanda kwa magoli 2-0 na kushika usukani wa Kundi A la michuano ya Kombe la Kagame la Castle kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana na kufanya timu zote nne zilizobaki za kundi hilo kuwa na nafasi sawa ya kutinga robo fainali.

Wekundu wa Msimbazi wenye pointi saba, watacheza mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi kesho dhidi ya timu inayoshika nafasi ya tatu, Red Sea ya Eritrea, yenye pointi sita baada ya jana mchana kuifunga Vital'O ya Burundi kwa goli 1-0 kwenye uwanja huo pia.


Zanzibar Ocean View inayoshika nafasi ya pili katika kundi hilo, ikiwa imelingana kwa kila kitu na Red Sea (lakini Ocean View wakiwa juu kwa kuwa walishinda 2-0 wakati timu hiyo mbili zilipokutana Jumanne), watamaliza hatua ya makundi kwa kucheza dhidi ya Vital'O walio katika nafasi ya nne wakiwa na pointi 4 baada ya mechi tatu.

Sare Jumapili inatosha kuzipeleka Simba, Ocean View na Red Sea kwenye robo fainali kutoka katika kundi hilo linalotoa timu tatu, lakini ni ushindi tu kwa Vital'O utakaoivusha timu hiyo ya Burundi kutoka katika hatua ya makundi.

Kiungo Haruna Moshi 'Boban' aliyerejea katika timu hiyo ya Msimbazi katika kipindi cha sasa cha usajili baada ya kukataa kuendelea kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Ligi Kuu ya Gefle IF ya nchini Sweden, alifunga kiufundi goli la 50 la michuano ya Kagame mwaka huu, baada ya kuuwahi mpira uliorudi baada ya kugonga 'mtambaa-panya' kufuatia kichwa cha Mohammed Banka, kabla ya kumpunguza beki mmoja na kuingia ndani na kupiga shuti kwa mguu wa kushoto lililoenda kutinga kwenye nyavu ndogo katika dakika ya 21.

Etincelles ambayo iliingia katika mechi ya jana ikiwa tayari imeshatolewa katika michuano hiyo baada ya kuwa ilishafungwa mechi zake zote tatu za kwanza, ilicharuka na kumaliza vizuri kipindi cha kwanza baada ya kunyanyaswa kwa muda mrefu.

Hata hivyo, hadi mapumziko, Simba ilipiga mashuti mawili tu yaliyolenga lango likiwemo lililozaa goli na mashuti manne tu 'yaliyopaa', dhidi ya shuti moja la wapinzani wao lililolenga lango na matatu ambayo yalienda pembeni. Simba ilitawala mpira kwa asilimia 51 dhidi ya 49 za wapinzani wao katika kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili, Simba walikuwa wakali zaidi huku wakionekana kuwa wazuri zaidi katika wingi zake mbili ambapo beki 'asiyechoka', Amir Maftah, alikuwa akipanda mfululizo kutokea upande wa kushoto na kusababbisha hatari nyingi kama ilivyokuwa kwa kwa Shija Mkina, Salum Machaku na mtokea benchi, Said Nassoro 'Cholo' waliokuwa wakiliandama lango la wageni kutokea upande wa kulia.

Mussa Hassan 'Mgosi' alifunga 'kiulaini' goli la pili kwa Simba jana na la 51 kwa michuano ya mwaka huu baada ya mechi 15, baada ya mabeki kumsahau katikati ya eneo la hatari kufuatia pasi ya beki mpya, Mganda, Derick Walulya, aliyekuwa akicheza mechi yake ya tatu kwa timu hiyo ya Msimbazi tangu alipojiunga nayo katika kipindi cha sasa cha usajili.

Kocha wa Simba, Mganda, Moses Basena, baada ya mechi hiyo kwamba ratiba 'iliyoshikana' inawaweka katika wakati mgumu wachezaji kwa sababu wanakosa muda wa kupumzika na akasikitika kuwapoteza nyota wake watatu walioumia ambao hawatacheza muda wote uliobaki ambao aliwataja kuwa ni kiungo, Ulimboka Mwakingwe, kipa mpya Mkenya, Wills Ochieng na beki, Kelvin Yondani.

Kocha wa Etincelles, Bizimanya Abdou, alisema timu yake haikuwa na maandalizi mazuri ndio maana wakafungwa mechi zote nne, lakini watafanyia marekebisho matatizo yote.

Yanga leo itaikabili Bunamwaya ya Uganda, wakati Elman ya Somalia itacheza El Mereikh ya Sudan katika mechi za mwisho za Kundi B zitakazochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, wakati mjini Morogoro nako kutakuwa na mechi mbili mbili za mwisho za Kundi C, ambapo vinara, Ulinzi ya Kenya, waliotoa kipigo cha 9-0 juzi dhidi ya Ports ya Djibouti juzi, watakabiliana na watetezi, APR ya Rwanda, huku pia St George ya Ethiopia ikicheza na Ports kwenye uwanja huo huo wa Jamhuri.