MNADHIMU Mkuu wa Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu(Pichani juu), amesema Serikali isipomshitaki Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), Chadema watafanya maandamano nchi nzima kushinikiza hatua hizo zichukuliwe.
Akizungumza nje ya Bunge jana, Lissu alisema ana ushahidi wa uhusika wa Chenge katika ununuzi wa rada ulioligharimu Taifa zaidi ya pauni milioni 28, alidai kuwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa inaruhusu Serikali kumchukulia hatua mbunge huyo.
Kwa mujibu wa madai ya Lissu, sheria hiyo ya Takukuru inaruhusu mtuhumiwa mwenye dalili za kushawishi rushwa, kushitakiwa mahakamani.
Mbunge huyo wa Chadema ambaye pia ni mwanasheria, alidai katika mchakato wa ununuzi wa rada hiyo, Chenge ndiye aliyeingia mkataba kati ya Tanzania na Kampuni ya BAE Systems iliyouza rada hiyo.
Alidai mbali na kuliweka Taifa katika hatari ya kupoteza fedha, Chenge pia kwa mujibu wa madai hayo, ndiye aliyeandika barua kwenda Benki ya Barclays iliyotoa fedha za mkopo kwa Tanzania kununulia rada hiyo.
Juzi wakati ujumbe wa Bunge ulipokuwa ukikabidhi ripoti ya kazi waliyofanya Uingereza ya kudai fedha hizo, kiongozi wa ujumbe huo, Naibu Spika, Job Ndugai, alisema Barclays ya Uingereza ndiyo iliyotoa fedha hizo, lakini kwa mkopo kwa hiyo ni deni la Tanzania.
Lissu pia alidai kuwa Chenge hajawahi kupinga hadharani, kwamba hana fedha hizo zaidi ya Sh bilioni moja nje ya nchi na wala hajawahi kupinga kumpa mshirika wake, Dk. Idris Rashid, pauni 600,000.
Alidai Chenge amewahi kutoa maelezo yanayokanganya kuhusu fedha hizo zilizoko nje ya nchi; mara ya kwanza kuwa amerithi na mara ya pili kuwa zimetokana na kazi yake ya ushauri wa kisheria.
Mbunge huyo alidai kuwa upo ushahidi kuwa Chenge hakuwahi kufanya kazi ya ushauri wa kisheria zaidi ya kuwa Mwanasheria Mkuu kwa muda mrefu, sheria ya Takukuru iliyopo ina kipengele cha kumtia hatiani.
Kipengele hicho kwa mujibu wa madai ya Lissu, kinaipa uwezo Serikali kumpeleka mahakamani Chenge kumhoji alipataje fedha hizo zilizoko nje ya nchi. (Source Habari Leo).

0 Comments