Mshambuliaji wa klabu ya Azam inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara na timu ya taifa, Taifa Stars, Mrisho Ngassa, ataondoka nchini Jumapili na kuelekea Marekani kufanya majaribio katika klabu ya Seattle Sounders.
Akiwa Marekani, Ngassa atapata nafasi pia ya kuichezea Sounders dhidi ya mabingwa wa England, klabu ya Manchenster United wakati wa mechi yao ya kirafiki itakayochezwa Marekani Julai 20.
Akizungumza na gazeti hili jana, kiongozi wa African Lyon, Rahim Kangezi, ambao ndio waliompa Ngassa nafasi ya kwenda kufanyiwa majaribio Marekani, alisema kwamba maandalizi ya safari ya nyota huyo wa Stars yamekamilika, ikiwemo viza ya kuingia Marekani.
Kangezi alisema kuwa wanaamini Ngassa ambaye amekuwa katika mazoezi na timu yake ya Azam inayojiandaa na Ligi ya Bara atafanya vizuri na ana nafasi kubwa ya kuingia mkataba na Seattle Sounders ambayo imekuwa ikimfuatilia mara kwa mara na kuridhika na kiwango chake.
"Kingine tunachoshukuru ni kupata dakika 15 za kuwavaa Manchester United ambayo ni moja ya timu kubwa duniani, tunafikiri kuwa Ngassa atafanya kile tunachokitegemea," aliongeza.
0 Comments