Wanawake walioathiriwa na ubakaji 

Mwanajeshi mwenye cheo cha Kanali anayeshutumiwa kwa ubakaji wa watu wengi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amejisalimisha kwa jeshi hilo.
Msemaji wa jeshi alisema Kanali Nyiragire "Kifaru" Kulimushi amejisalimisha pamoja na zaidi ya wapiganaji wake 150, wanaoshutumiwa pia kwa ubakaji wa wanawake wengi.
Mwezi uliopita, takriban wanawake 100 waliwashutumu waliokuwa waasi waliojiunga na jeshi la nchi hiyo kwa kuwadhalilisha kijinsia katika jimbo la Kivu ya Kusini.

Ujumbe wa umoja wa mataifa mwaka jana umeelezea nchi hiyo ya Congo kama "mji mkuu wa ubakaji duniani".
Ghasia zilizodumu miaka 16 mashariki mwa Congo zimesababisha kuenea kwa udhalilishaji wa wanawake na watoto wa kike.
Msemaji wa jeshi Lt Kanali Vianney Kazarama ameiambia BBC kuwa Kanali Kifaru alijisalimisha baada ya kutoka misituni kwenye ngome yake iliyopo mashariki mwa Congo.
Alisema, "walikuwa 150, na silaha zao-zikiwemo silaha nzito".