Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), jana walirushiana vijembe mbele ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu ujenzi wa barabara kutoka Kigoma hadi Nyakanazi, mkoani Kagera kwa kiwango cha lami.
Tukio hilo lilitokea wakati wa hafla ya ufunguzi wa barabara ya Mwandiga hadi Manyovu mkoani Kigoma iliyojengwa kwa kiwango cha lami kwa fedha za Serikali ya Tanzania Shilingi bilioni 60. Hafla hiyo ilifanyika katika mji mdogo wa Mwandiga.
Zitto ndiye aliyekuwa wa kwanza kurusha vijembe hivyo alipopewa nafasi ya kuwasalimia wananchi waliohudhuria hafla hiyo.
Baada ya kupewa fursa hiyo, Zitto alisema kuwa bado hakubaliani na msimamo wa Waziri Magufuli wa ujenzi wa barabara hiyo kuanzia Nyakanazi ambayo ni sehemu ya Mkoa wa Kagera.
Mbunge huyo alisema kuwa Nyakanazi siyo sehemu ya Mkoa wa Kigoma na viongozi na wananchi wa Mkoa wa Kigoma ndiyo wenye shida na kiu ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Kutokana na kutoridhishwa na suala hilo, Zitto alimuomba Rais Kikwete kuangalia upya ili ujenzi huo uanzie Kigoma.
Mbunge huyo alisema kuwa Waziri Magufuli aliwahi kujibu swali bungeni na kusema kuwa yeye (Magufuli) ni sawa na kinyozi na kwamba anayo mamlaka na madaraka ya kuona wapi panafaa kuanzia ujenzi wa barabara hiyo jambo ambalo alisema sio sahihi.
"Waziri Magufuli asifananishe barabara na kichwa hivyo ni vitu viwili tofauti, barabara ndiyo uchumi wa Mkoa wa Kigoma na ipo kila sababu ya barabara hiyo kuanza kujengwa kuanzia Kigoma badala ya Nyakanazi ambayo ni sehemu ya Mkoa Kagera," alisema Zitto.
Akijibu kauli za Zitto, Dk. John Magufuli alisema kuwa ujenzi wa barabara nchini haufanywi kwa kuangalia jimbo ni la nani, bali hufanywa kwa maslahi ya Watanzania wote na ndiyo maana barabara hiyo inajengwa kwa maslahi ya Watanzania.
Waziri Magufuli alisema kuwa hawako hapo kwa ajili ya kugombania barabara inaanzia wapi bali jambo la muhimu ni kuona kwamba barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami na inakamilika ili wananchi wote wafaidi matunda yake.
Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema kuwa wananchi wa Jimbo la Kigoma Kaskazini wamemchagua Zitto kuwa mbunge wao, lakini pamoja na hilo Zitto hana serikali, bali Serikali ni ya Chama Cha Mapinduzi haina kinyongo kwa yoyote.
Alisema ndiyo maana licha ya kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM, imeamua kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wote bila kinyongo wala ubaguzi.


0 Comments