Mwanamuziki maarufu wa muziki wa kufokafoka (Hip Hop) nchini Senegal Omar Toure, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Rais Abdoulaye Wade, amekamatwa.
Mwandishi wa BBC Thomas Fessy mjini, Dakar, anasema washabiki wake kadhaa wameandamana wakitaka aachiliwe huru.
Polisi hawakutoa sababu za kukamatwa kwa Bw Toure, ambaye ni maarufu kwa jina la Thiat.
Alizungumza katika mkutano wa hadhara wa wapinzani siku ya Jumamosi na kutaka Bw Wade asigombee tena katika uchaguzi ujao mwakani.

Viongozi kadhaa wa upinzani waliungana na washabiki nje ya mahakama kuu mjini Dakar wakitaka aachiliwe huru, mwandishi wa BBC anasema.
Walisema kukamatwa huko ni dalili za mwisho za kuongezeka kwa ukandamizaji nchini Senegal kuelekea uchaguzi ujao.
'Sasa inatosha'
Bw Toure ni mwanachama wa kundi la ‘Inatosha Bendi.’
Mwezi January alisaidia uzinduzi wa vuguvugu la ‘Enough is Enough’ ambalo linawahamasisha vijana kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi.
Wiki iliyopita serikali ilipiga marufuku maandamano ya kisiasa katikati mwa mji wa Dakar.
Mwezi uliopita vurugu zilizuka katika mji huo, liliochagizwa na pendekezo la Rais Wade kubadili katiba.
Alitaka kupunguza asilimia ya kura zinazohitajika kushinda uchaguzi wa Urais na kuepuka duru ya pili ya uchaguzi kutoka zaidi ya asilimia 50 kwenda asilimia 25%.
Bw Wade – ambaye alishika madaraka katika uchaguzi miaka 11 iliyopita, aliachana na pendekez hilo lakini anatarajia kuwania urais tena kwa awamu ya tatu katika uchaguzi wa mwakani.
Upinzani unasema hatua hiyo itakuwa kinyume na katiba na wanadai aondoke madarakani.