Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika.

Wanaharakati sita waliohusika kuandaa maandamano ya kuipinga serikali nchini Malawi wamekimbia kujificha wakiogopa vitisho kwamba watakamatwa.
"Nitawaua," Rais Bingu wa Mutharika amewaonya wahusika sita siku ya Ijumaa.
Mmoja wao, Rafiq Hajat, ameiambia BBC amejificha na kuwa ‘maisha yake ni mafichoni,’
Watu 19 waliuawa wakati wa maandamano ya siku mbili wiki iliyopita dhidi ya kupanda kwa gharama za maisha nchini Malawi.
Bw Mutharika alisambaza wanajeshi katika mji mkuu, Lilongwe, mji mkubwa kibiashara, Blantyre, na Mzuzu ulioko Kaskazini kudhibiti maandamano hayo. Rais anawatuhumu waandamanaji kwa kufanya uhaini.

‘Tunaupa changamoto mtazamo wa kimsingi kabisa wa utamaduni nchini Malawi ambapo mtu hawezi kuthubutu kuikosoa serikali,’ alisema Rafiq Hajat, Mkurugenzi wa Taasisi ya Malawi ya Mawasiliano ya Kisera.
"Mkirudi tena mitaani, nitawaua. Sasa imetosha!" Bw Mutharika alisema, baada ya kutaja majina sita ya watu walioandaa maandamano kwenye hotuba yake kwa polisi.
Watu hao ni pamoja na Bw Hajat, Mkurugenzi wa kundi la uhamasishaji katika Taasisi ya Uhusiano wa Kisera ambaye amezungumza na BBC akiwa mafichoni akiohofia usalama wake.
"Mke wangu na watoto wana wasiwasi. Wnahofu kuhusu usalama wangu na wa kwao. Hakuna mtu yeyote anayekaa nyumbani, " amekiambia kipindi cha BBC Network Afrika.
"Mama yangu amefanyiwa upasuaji wa moyo mara tatu. Anaonekana amezeeka miaka kumi zaidi katika kipindi cha siku chache."
Bw Hajat alisema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kamati ya ushauri ya Haki za Binadamu nchini Malawi, McDonald Sembereka, alikuwa mmojawapo watu waliojificha huku akijua kuwa, Mwenyekiti Undule Mwakasungula, amekimbia Malawi.
Alisema wanaharakati hawawezi kukandamizwa na wataendelea kuratibu maandamano zaidi iwapo madai yao hayatatekelezwa.