Karibu maafisa polisi waandamizi 700 nchini Misri wamefukuzwa kazi kutokana na mauaji ya waandamanaji wakati wa mapinduzi ya kiraia mapema mwaka huu.
Waziri wa Mambo ya Ndani Mansour Essawy amesema utumishi wa majenerali 505 na maafisa 164 utakoma ifikapo Agosti Mosi mwaka.
Uamuzi huo umekuja wakati waandamanaji katika uwanja wa wazi wa Tahrir mjini Cairo wakishinikiza kesi za maafisa wa polisi na maafisa wa serikali wanaohusishwa na ufisadi wakati wa utawala wa Mubaraka zifanyiwe maamuzi haraka.
Jeshi limethibitisha pia kuwa kura zilizokuwa zipigwe mwezi Septemba zimeahirishwa.
"Imeamriwa kusitisha kwanza uchaguzi wa bunge mwezi Oktoba au Novemba," afisa mmoja kutoka baraza la kijeshi la mpito la Misri ameliambia shirika la habari la Taifa Mena siku ya Jumatano.
Vyama vingi vipya vya kisiasa nchini Misri vimetaka upigaji kura ucheleweshwe ili viweze kujipanga kushindana dhidi ya vile vilivyo na mtandao mzuri na vikundi vingine vyenye nguvu ya upinzani, hasa cha Muslim Brotherhood.
Siku ya Jumanne, jeshi lilisema lingeweka kanuni ambazo zitaongoza uteuzi wa wajumbe 100 watakaoandika katiba mpya ya Misri. Hiyo inaweza kuongeza ugumu kwa kundi lolote lenye msimamo mkali wa kiislam kuchagua bunge na kisha kulitumia hilo kama njia ya kupata uongozi unaogemea sharia za kiislam, mchambuzi anasema.
'Mtikisiko mkubwa'
Wakati maandamano katika uwanja wa wazi wa Tahrir unaingia siku ya sita, wizara ya mambo ya ndani ambayo ndio inasimamia huduma ya usalama ambayo kwa sasa inachukiwa sana, wakijulikana kwa ukatili wao wakati wa utawala wa Mubarak, imezindua kile inachokiita ‘mtikisiko mkubwa katika historia ya jeshi la polisi.’
Kati ya hao waliofukuzwa kazi wako mameja jenerali 505 wakiwemo wasaidizi wakuu10 wa waziri wa mambo ya ndani, makanali 82, na mabrigedia 82 ripoti zinasema.
Televisheni ya Taifa ya Misri imesema maafisa 37 kati ya waliofukuzwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya waandamanaji.
Zaidi ya waandamanaji 800 waliuawa wakati wa siku 18 za protesters mapinduzi ya kiraia yaliyosababisha kuondoka madarakani kwa Rais Hosni Mubarak Februari 11.
Uamuzi huo unaonekana kuwa ushindi kwa Waziri mkuu wa Misri Essam Sharaf ambaye anapata changamoto, anasema mwandishi wa BBC Jon Leyne mjini Cairo. Tangazo la awali la Waziri mkuu la kuchukua hatua kama hizo lilizuiliwa na waziri wa mambo ya ndani.
Waandamanaji wameapa kushinikiza utawala wa kijeshi wa Misri. Wanataka serikali mpya, yenye mamlaka yanayodhibitiwa na baraza la kijeshi, kuachiliwa kwa raia wanaoshikiliwa na mahakama za kijeshi na kuharakisha kesi za maafisa wa utawala uliopita.
0 Comments