Balozi wa Finland bwana Juhan Toivoven akimkabidhi kitabu cha sifa za utalii nchini Tanzania makamu wa rais Dr,Bilal Mohamed wakati alipofika katika ofisi za makamu wa rais ili kumuaga kwani ameshamaliza muda wake wa kazi nchini Tanzania.
Makamu wa rais akimsikiliza kwa makini aliyekuwa balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Dr,Guido Herzi pindi alipofika ofisini kwake akitaka mkono wa baraka kwa kurejea kwao Ujerumani mara baada ya kumaliza kipindi cha kufanya kazi nchini Tanzania kumalizika.(Picha toka kwa John Bukuku)

MABALOZI wa Finland na Ujerumani, jana waliagana na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal huku wakielezea kubakia na kumbukumbu ya namna Watanzania wanavyoishi na walivyowathamini wakati wakifanya kazi za kidiplomasia nchini.

Wa kwanza kufika ofisini kwa Makamu wa Rais Ikulu Dar es Salaam, alikuwa Balozi Juhan Toivonen wa Finland aliyeisifia Tanzania na kumzawadia Makamu wa Rais kitabu cha “The Great Savanna.”



Kitabu hicho kina vivutio kadhaa vya utalii nchini Tanzania na kilichapishwa kwa Kifinland na kisha kutafsiriwa kwa Kiingereza.


Balozi huyo alimuahidi kutoa nakala nyingine za kitabu hicho zipatazo 9,000 kwa Makamu wa Rais ili zisambazwe kwa wadau wa utalii nchini.


Naye Makamu wa Rais licha ya kumshukuru Balozi Toivonen, alifafanua kuwa uhusiano wa Finland na Tanzania ni wa siku nyingi na wenye tija na kwamba historia inaonesha kuwa katika fani ya Jiolojia, Finland imesaidia katika kutanua rasilimali watu nchini.


Katika hatua nyingine, Balozi huyo alitaka kujua namna Tanzania inavyomudu kutanua demokrasia kulinganisha na mataifa mengine ya Afrika.


Makamu wa Rais alimjibu kuwa hali hiyo inatokana na uhusiano chanya kati ya Serikali na wananchi na akatilia mkazo juu ya uongozi uliotukuka wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere hasa katika vigezo vya kujenga ushirikiano na hali ya kukubaliana kama Watanzania.


Naye Balozi wa Ujerumani, Dk. Guido Herz aliyekaa nchini kwa miaka mitatu, alisifu makubaliano ya kupatikana amani ya kudumu Zanzibar huku akifafanua kuwa namna alivyoona tatizo lililokuwepo, lakini akiamini lingetatuliwa na wananchi wenyewe.


Alifafanua pia kuwa anaamini demokrasia inakua nchini na pia akaeleza kuwa siasa za Tanzania, bado zina mizizi ndani ya Chama Cha Mapinduzi.


Dk. Bilal alimuelezea Balozi huyo namna Tanzania ilivyojipanga katika sekta ya utalii huku ikiwaza kuwa na utalii wenye tija, lakini usiokuwa na idadi ya watalii wanaofurika na hivyo kuharibu mazingira.


Suala lingine lililojadiliwa lilikuwa juu ya uchimbaji wa madini ya urani huku Makamu wa Rais akifafanua kuwa, kazi hiyo itafanywa kwa uwazi kabisa na tayari hatua za awali za kujitathmini kabla ya kuanza kazi hiyo zimeanza zikiwa chini ya wizara zinazohusika na madini sambamba na Sayansi na Teknolojia.

.