Chancela wa Ujerumani Angela Merkel ametangaza kuwa serikali yake itachangia pesa kusaidia juhudi za kukabiliana na ukame Afrika Mashariki
Bi Merkel amesema serikali yake itatoa Euro 1 million katika mfuko wa kusaidia walioathirika na njaa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kulingana na Umoja wa Mataifa zaidi ya watu milioni 10 wanakabiliwa na njaa kufuatia kipindi kirefu cha ukame na wanahitaji misaada ya dharura.

Walioathrika zaidi ni raia wa Somalia, nchi ambayo imekumbwa na vita kwa zaidi ya miaka 20.
Chancela wa Ujerumani ametangaza mchango huo katika mkutano kati yake na Rais Mwai Kibaki mjini Nairobi ambapo ameanza ziara rasmi ya nchi tatu barani Afrika.
Raia wengi wasomalia walioathirika na njaa wameingia nchini Kenya ambapo wamepewa hifadhi katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab, kaskazini mwa nchi hiyo.
Katika ziara yake, Bi Merkel atajadili jinsi ya kuwa na ushirikiano wa kiuchumi hususan sekta ya nishati.
Ujumbe wa viongozi wa kibiashara unaandamana na Bi Merkel wakati akizuru Kenya, Nigeria na Angola.
Kabla ya ziara yake, alisema nia yake ni kutembelea mataifa matatu yenye uchumi mkubwa, lakini ambayo yamekuwa na msukosuko wa kisiasa.
Bi Merkel amesema Ujerumani itayasaidia kuleta uthabiti wa kisiasa ili kufanikisha mfumo wa demokrasia.
Chancela huyo amehimiza mwenyeji wake, Rais Kibaki ahakikishe kuwa suala la rushwa linakabiliwa vilivyo na mfumo wa utawala bora na demokrasia unashika mizizi nchini Kenya.
Bi Merkel pia ametangaza kuwa taasisi za Ujerumani zitasaidia Kenya katika maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2012kuhakikisha kuwa utakuwa wa haki na kweli.
Ujerumani imeahidi kutoa Euro milioni 140 kusaidi katika kusambaza huduma za kijamii nchini Kenya hasaa ilioambatana na malengo yamilenia.
.