Waziri wa habari,vijana, utamaduni na michezo Dr,Emmanuel Nchimbi.

SERIKALI imevionya vyombo vya habari kujiepusha na uchochezi unaofanywa na vikundi vya kisiasa, kwa kuwa hatima ya matukio ya aina hiyo ni kusababisha maafa kwa taifa.

Onyo hilo lilitolewa bungeni jana na Waziri wa Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni, Dk. Emmanuel Nchimbi, alipokuwa akifanya majumuisho ya Makadirio ya Matumizi ya Wizara yake kwa ajili ya mwaka wa fedha wa 2011/12.

Alisema kwa kuwa tayari vyombo vya habari nchini vimejijengea heshima, ni vyema vikafanya kazi kwa weledi ili kudumisha amani na mshikamano wa Watanzania, badala ya kuwachochea na kuwachonganisha kwa manufaa ya watu wachache au vikundi.

“Utakuta mwanasiasa anasema hatukubali…tutamwaga damu, nawe mwandishi au chombo cha habari unarudiarudia kauli hizo, huo si uzalendo.

Jamani huu ni uchochezi… inawezekana baadhi wakafurahi, kwamba wanafanya vizuri sokoni kwa kuandika habari za aina hii ambazo nyingine ni za uchochezi.



“Nasema hivi, mchezo wao ni maafa kwa Taifa hili. Watu wanaviamini sana vyombo vya habari, sasa isifike mahali baada ya kuwaaminisha vitu vya ajabu, yakaibuka ya kuibuka.

Eleweni kwamba kwa kuwa wanawaamini, hiyo ni heshima kubwa, itumieni fursa hiyo hiyo kuijenga nchi kwa kusisitiza amani na uzalendo,” alisema.


Hata hivyo, alisema uzalendo hauna maana ya kupendelea Serikali, bali kuandika mambo ya kweli, yenye kuchochea maendeleo na ustawi wa nchi.

Waziri alisema wizara yake ilidhamiria kwa dhati kushirikiana na wadau wote wa habari katika kuweka mazingira endelevu yatakayowezesha kuwapo ukuaji zaidi wa uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Alishukuru pia kwa michango na hoja za kuboresha utendaji wa wizara kuanzia sekta ya
habari, maendeleo ya vijana, michezo na utamaduni.

Bunge liliidhinisha jumla ya Sh bilioni 18.5, kati ya hizo, Sh bilioni 3.8 zikiwa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.