JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni, linawashikilia askari wanne wa kituo cha Polisi cha Magomeni kwa mahojiano zaidi, kutokana na tukio la kutoroka kwa mahabusu 13 kituoni hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela,(Pichani juu) alisema jana kuwa mahabusu walipata mwanya wa kuwatoroka askari hao baada ya kukatika umeme usiku wa kuamkia Jumanne wakati mahabusu hao wakila chakula walichopelekewa na ndugu zao.
Kenyela alisema tukio hilo halijawahi kutokea na kuongeza kwamba lazima lichunguzwe kwa makini kugundua kama kulikuwa na uzembe uliofanyika ili askari waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria.
“Tukio hili la kukimbia mahabusu si jambo la kawaida kwa sababu halijawahi kutokea na ndio maana ninasema lazima tuchunguze kwa makini, tujue kama kulikuwa na uzembe wa askari waliokuwa lindo ili wachukuliwe hatua kali,” alisema Kenyela na kuongeza:
“Lakini tumebaini mahabusu waliotoroka ni 13 na sio 27 kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vilininukuu juzi wakati sikuzungumza navyo kabisa.”
Aliwataja mahabusu waliotoroka kuwa ni Abdallah Said (29), mkazi wa Mansese; Bakari Athumani (45) mkazi wa Mburahati; Omari Hamad (45) mkazi wa Mburahati; Robeth Annastazius (28) mkazi wa Magomeni; Abdallah Masud (23) Mkazi wa Magomeni; Wakati Hadji (23) mkazi wa Tandale na Usuguli Devid (24), mkazi wa Tegeta,
Wengine ni Abubakari Salum (34) mkazi wa Mansese; Hemed Athumani (23) mkazi wa Magomeni; Jumanne Tawanya (27) mkazi wa Magomeni; Matunguli William (26) mkazi wa Kigogo; Edward Maleko (22) mkazi wa Magomeni na Hemed Hassan (19), mkazi wa Magomeni.
Alisema kati ya mahabusu hao ni mmoja (Wakati Hadji), ndiye aliyekamatwa huku juhudi za kuwatafuta wengine zikiendelea.
Aliongeza kuwa kati ya makosa waliyokuwa wakituhumiwa nayo mahabusu hao ni wizi, kujeruhi, kuvunja na kupora.
Aidha, Kenyela alitoa wito kwa wananchi kusaidia kutoa taarifa kama wakiwaona mahabusu hao.
CHANZO: NIPASHE